UJUMBE: 64-0213 Ndipo Yesu Akaja Na Kuita
Mpendwa Bibi-arusi Neno,
Tunaishi katika saa zenye giza kuliko, lakini sisi HATUNA HOFU, Bwana amekuja. Amekuja kulitimiza Neno Lake katika siku ya mwisho. Jinsi Alivyokuwa wakati huo, ndivyo Alivyo leo. Jinsi udhihirisho na utambulisho Wake ulivyokuwa wakati huo, ndivyo ulivyo leo. Yeye angali ni Neno la Mungu, akijidhihirisha Mwenyewe katika mwili wa kibinadamu katika malaika Wake wa saba mwenye nguvu na ametufunulia, sisi ni Bibi-arusi Neno lililo Hai Wake.
Hatuna muda wa kujadiliana au kuzozana; tumepita wakati huo; tunasonga mbele, inatupasa kufika kule. Roho Mtakatifu amekuja miongoni mwetu. Bwana Yesu katika umbo la Roho amejifunua na kujidhihirisha Mwenyewe kupitia nabii Wake kwamba Yeye ni Sauti ya Mungu kwa Bibi-arusi Wake.
Yeye alisema angekuja. Alisema angefanya jambo hili. Alisema angejitokeza jukwaani katika siku za mwisho na kufanya mambo haya kama alivyofanya alipokuja katika mwili mara ya kwanza, Naye huyu hapa akilifanya jambo hilo. Mnaogopa nini? HAKUNA!!!
Tumo njiani kuelekea Utukufuni! Hakuna kitu kitakachotukomesha. Mungu atalithibitisha Neno Lake. Sijali ni kitu gani kitakachotukia. Wakati wa matendo umefika. Wakati wa kuamini ama kutokuamini umefika. Ule Mstari wa kutengana ambao huwajia kila mwanamume na mwanamke umewasili.
Wewe ulizaliwa kwa kusudi fulani. Wakati Nuru ilipokumulika, iliondoa giza lote ndani yako. Wakati ulipoisikia Sauti Yake ikizungumza nawe kwenye kanda, jambo fulani lilitendeka. Ilinena na nafsi yako. Ilisema, “Bwana amekuja na anakuita. Usifadhaike, usiogope, Ninakuita. Wewe ni Bibi-arusi Wangu”.
Enyi watu, iweni na hakika! Msibahatishe tu nusunusu kuhusu hilo. Mungu anao mpango: Neno Lake alilolirekodi kwenye kanda. Bwana amekuja na anawaita. Njooni kwenye njia ya Mungu iliyoandaliwa.
Bwana atamuunganisha kwa mara nyingine tena Bibi-arusi Wake kote ulimwenguni na Sauti Yake. Atatutia moyo, atatuhakikishia, atatuponya, atatuleta katika Uwepo Wake mkuu na kutuambia:
Bwana amekuja na anakuita. Loo, ewe mwenye dhambi, loo, ewe mgonjwa, hivi huoni Bwana aliyedhihirishwa katika mwanadamu, katikati ya waamini? Yeye amekuja kuwaita watoto Wake wanaoamini wapate afya. Amekuja kumwita mwenye dhambi apate kutubu. Ewe uliyerudi nyuma, mfuasi wa kanisa, Bwana amekuja na anakuita.
Ni kumwagwa kwa Roho Wake Mtakatifu kulikoje ambako Bibi-arusi atakuwanako Jumapili hii Mungu atakapowakusanya watoto Wake pamoja Kwa mara nyingine tena na kuingia katika nyumba zetu, makanisa yetu, mikusanyiko yetu, na kutuita na kusema, “Bwana amekuja na anawaita. Chochote mnachokihitaji, ni chenu.”
Hebu maneno hayo na yaingie ndani ya mioyo yenu, ndugu na dada. CHOCHOTE MNACHOKIHITAJI, BWANA AMEKUJA NA KUWAPENI JAMBO HILO.
Baba wa Mbinguni, Ee Bwana, jalia litukie tena. Mambo yote hayo ambayo nimesema, “Yesu amekuja na anakuita.” Yeye hufanya nini hapo anapokuja? Huita. Na jalia litendeke tena, Bwana. Jalia Roho Wako Mtakatifu aje miongoni mwa watu usiku wa leo, Bwana Yesu katika umbo la—la Roho. Jalia aje usiku wa leo na ajifunue Mwenyewe, halafu ajidhihirishe Mwenyewe.
Ndugu Joseph Branham
Ujumbe: 64-0213 Ndipo Yesu Akaja Na Kuita
Saa: 6:00 MCHANA masaa ya Jeffersonville(ni saa 2:00 USIKU ya Afrika Mashariki)
Maandiko:Yohana Mt. 11:18-28