24-0414 Makao Ya Baadaye Ya Bwana Arusi Wa Mbinguni Na Bibi-Arusi Wa Duniani

UJUMBE: 64-0802 Makao Ya Baadaye Ya Bwana Arusi Wa Mbinguni Na Bibi-Arusi Wa Duniani

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Chumvi ya dunia,

Ee Bibi-arusi mpendwa, tunakuwa na wakati ulioje, tumeketi pamoja katika ulimwengu wa roho, katika uwepo wa Neno, tukikomaa, tukijitambua sisi ni nani, tunatoka wapi, na wapi tunakoenda.

Kujua, kutoka katika vilindi vya mioyo YETU, hivi SASA sisi ni wana na binti za Mungu. Si ati tutakuwa, tupo SASA HIVI. Sisi ni sifa za mawazo ya Mungu.

Shetani anapotushambulia, na kujaribu kutuonyesha makosa yetu, maisha yetu ya nyuma, na kushindwa kwetu kwa kila siku; anapojaribu kutuvunja akilini mwetu na rohoni kwa uwongo wake, tunamkumbusha tu na kumwambia, “Mungu, tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, aliniona mimi; hiyo ni kweli ewe Shetani, MIMI, naye akamtuma Yesu kunikomboa MIMI.” PIGA!

“Sasa Shetani, niache, kwa maana Damu ya Mwanawe yanena kwa ajili YANGU. Siwezi kutenda dhambi. Kukosea kwangu, ndio, makosa yangu mengi, hayo hata hayawezi kuonekana na Mungu. Kitu pekee Anachosikia ni sauti YANGU ikimuabudu na kumsifu Yeye, na kitu pekee Anachokiona ni uwakilisho WANGU.”

Uwakilisho wetu unatukusanya kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, na kutuunganisha chini ya Neno aliloliandaa kwa ajili ya Bibi-arusi Wake kwenye kanda. Ndilo jambo pekee atakaloliheshimu; kwa maana ndio Njia yake Yeye aliyoiandaa.

Anaenda kutuambia nini na kutufunulia kitu gani baadaye? Tumemsikia Yeye akinena kupitia nabii Wake mara nyingi sana akituambia kuhusu jinsi gani Makao yetu mapya yatakavyokuwa, lakini wakati huu itakuwa kana kwamba hatukuwahi kusikia lolote kulihusu wakati wowote ule.

Mjenzi wa Kiungu ameubuni huu kwa ajili ya mpendwa Wake. Mnaona? Loo! ni mahali pa jinsi gani, wakati, Tabia ya Mungu, Mjenzi Hodari wa Kiungu ameubuni kwa ajili ya sifa za Kiungu ambazo zimechaguliwa Kiungu tangu zamani na Mungu Mtakatifu Ambaye—Ambaye ndiye Mwanzilishi wa Uzima wa Mungu! Huo Mji utakuwaje! Wazia jambo hilo.

Hatuwezi kujizuia. Kuchangamshwa kwetu na matarajio yetu yapo kileleni. Mioyo yetu inaenda mbio kumsikia Mungu akinena nasi moja kwa moja na kutuambia kuwa hivi sasa anaandaa na kuyabuni Makao yetu mapya ili tuweze kuishi Milele yote pamoja Naye.

Tutasikia kipi kingine, na kitu gani kitakachofunuliwa kwetu Jumapili, Wakati anapotuambia kila kitu kuhusu Kuchaguliwa tangu zamani, Uwakilisho, Kipindi cha wakati, Siku ya Nane, Mlima Mtakatifu, Piramidi, na Kusanyiko Takatifu?

Je, tunaweza kuyafunga mawazo yetu kote kwa yale yanayotokea hivi sasa? Mungu anamkusanya Bibi-arusi Wake kutoka ulimwenguni kote ili aweze kutuambia jinsi gani Makao yetu mapya yatakavyokuwa. Yeye atatuambia kwa undani kila taarifa ndogo. Tutakuwa na wakati uliotukuka jinsi gani.

Kwa upande mwingine, vita vyetu havijawahi kupungua makali. Shetani anatushambulia kuliko wakati mwingine wowote. Mashambulizi yake hayaonekani kuwa mepesi ama kuondoka.

Lakini UTUKUFU kwa Mungu, IMANI yetu katika Neno lake haijawahi kuinuliwa kama hivi. IMANI yetu ya kujijua sisi ni nani imetia nanga ndani kabisa ya Nafsi yetu, hata hatuwezi kutetereka.

Sisi HATUNA cha kuogopa; HAKUNA cha kuhofia. Baba Yeye ndiye anayehusika kwa ajili yetu kikamilifu. Anatuongoza na kutuelekeza KILA HATUA ZETU. Ametushika katika kiganja cha Mkono Wake. Shetani ni mwongo tu ambaye mwisho wake uko karibu, naye anajua hilo. Yeye ndiye anayeogopa, anajua anashughulika na Bibi-arusi-Neno Lililonenwa wa Mungu naye hushindwa kila wakati.

Sisi NI NENO. Tulikuwa ndani yake tangu mwanzo. Si kwamba tutakuwa hivyo siku moja, TUKO HIVYO SASA HIVI. Ikiwa sisi ni Neno, basi tunaweza KUNENA NENO, IKIWA TU TUTAAMINI… NASI TUNAAMINI.

Wewe ni aidha mwamini (NENO) ama wewe ni mwenye mashaka (SI NENO). Hakuna hata kiungo kimoja katika miili yetu kisichoamini Neno moja. Haya basi! Tumemthibitishia Shetani hivi punde: sisi ni Neno. Twaweza kuwa ngozi iliyo chini ya unyayo, LAKINI BADO TU SEHEMU YA ULE MWILI!!!

Kwa hiyo wakati huyo mwongo anapomjia mmoja wetu, Bibi-arusi anakusanyika kutoka ulimwenguni kote nasi TUNAMPIGA na KUMPIGA kwa Neno.

Ugonjwa unapomjia mmoja wetu, sisi huungana pamoja na KUMPIGA! Wakati mmoja wetu apatapo kujisikia kudhoofu na kushushwa moyo, sisi sote hufanya kitu gani? HUMPIGA!

Tunaenda Nyumbani, Ewe Bibi-arusi. Wakati umefika. Bibi-arusi amejiweka mwenyewe tayari. Tuko ndani ya Safina. Yeye Amefunga mlango nasi tuko ndani salama. Tunaweza kusikia muziki wa Bibi-arusi ashuke akitembea kwenye safu kuungana na Bwana-arusi.

Tutakuwa kwenye fungate yetu kwa miaka 1000, kisha tutaenda pamoja na kila mmoja na Yeye kwenye Makao yetu ya Baadaye.

Msilikose, Enyi marafiki. Kuna njia moja tu iliyoandaliwa na kuthibitishwa na Mungu: KANDA. Ni Nguzo ya Moto ikinena na kumwongoza Bibi-arusi Wake.

Lolote ufanyalo, iweke Sauti hiyo mbele yako na familia yako Jumapili hii. Imani chanzo chake ni kusikia, kulisikia Neno, na Neno huja kwa nabii. Roho Mtakatifu ni Nabii wa siku yetu akinena na Bibi-arusi Wake kwa Kanda.

Mnakaribishwa kuungana nasi Jumapili hii saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,( ni saa 1:00 MOJA JIONI ya Afrika Mashariki ) wakati sehemu ya Bibi-arusi watakapoungana pamoja kumsikiliza Mungu, wote kwa wakati mmoja, akinena kupitia malaika Wake mwenye nguvu akituambia yote kuhusu: Makao Ya Baadaye Ya Bwana Arusi wa Mbinguni na Bibi-arusi wa Duniani 64-0802.

Ndugu. Joseph Branham