Category Archives: Uncategorized

25-1130 Kile Kipeo

UJUMBE: 64-0705 Kile Kipeo

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Kipeo Cha Mungu,

Uhai wote wa kweli uliokuwemo Katika ubua, kishada, na ganda, sasa unakusanyika ndani yetu, Uzao wa Kifalme wa Mungu, Vipeo Vyake, nasi tuko kwa ufufuo, tayari kwa mavuno. Alfa imekuwa Omega. Ya kwanza imekuwa ya mwisho, na ya mwisho sasa ndiyo ya kwanza. Tumepitia hatua fulani nasi tumekuwa Vipeo Vyake, kipande kilichokatwa kutoka Kwake.

Bibi-Arusi na Bwana-Arusi ni Mmoja!

Mungu alimwonyesha nabii Wake kule kuonekana kimbele kwa kila mmoja wetu tupate kukaguliwa, Vipeo Vyake, katika ono. Aliposimama pale na Bwana akimtazama Bibi-Arusi akipita mbele yake, Yeye Alimwona kila mmoja wetu. Sisi SOTE macho yetu yalikuwa yameelekezwa MOJA KWA MOJA KWAKE YEYE. Alisema tulikuwa watu walio wazuri mno aliopata kuwaona maishani mwake. Tulikuwa na madaha. Tulionekana wazuri mno kwake.

Kumbukeni, hili lilikuwa ni ONO la Bibi-Arusi; vile angeonekana, na kutuambia hasa kile alichokuwa akifanya. Sikilizeni kwa makini.

Yeye atatoka katika mataifa yote, kumkamilisha Bibi-arusi. Kila mmoja wao alikuwa na nywele ndefu na bila kujipodoa, nao ni wasichana wazuri sana. Nao walikuwa wakinitazama. Hao waliwakilisha Bibi-arusi akitoka katika mataifa yote. Mnaona? Yeye…Kila mmoja wao aliwakilisha taifa moja,* walipokuwa wakipiga hatua kikamilifu kulingana na Neno.

Bibi-Arusi, Hebu niliseme hilo tena, BIBI-ARUSI, kutoka kila taifa ati walikuwa wameyaelekeza macho yao kwa mchungaji wao, kundi la watu….HAPANA, hivyo sivyo alivyosema. Wao walikuwa wameyaelekeza macho yao KWA NABII, wakimtazama yeye.
Mradi tu waliyaelekeza macho yao kwa nabii, walikuwa wakipiga hatua kikamilifu. Lakini Kisha yeye anatuonya, jambo fulani lilitukia. Baadhi yao waliyaondoa macho yao kwake na kuanza kuangalia kitu kingine ambacho kiliingia katika machafuko matupu.

Halafu, yanipasa kumwangalia. Atakosa kupiga hatua kwa utaratibu wa hilo Neno nisipomwangalia, wakati anapopita, kama atanikaribia. Labda itakuwa wakati wakati wangu utakapokwisha (mnaona?), nitakapomaliza mwendo, ama cho chote kile.

Yampasa amwangalie, la sivyo atakosa kupiga hatua taratibu wakati anapopita. Lakini kisha anasema labda itakuwa ni wakati wangu, nitakapomaliza mwendo, wakati sipo hapa, Wanaweza kukosa kupiga hatua taratibu kwa kutoyaelekeza macho yao kwake.

Alikuwa akimwonya BIBI-ARUSI waziwazi, Hamna budi kuyaelekeza macho yenu kwenye Sauti ya Mungu iliyo kwenye kanda. Hiyo ndiyo njia iliyoandaliwa na Mungu ya siku hii. Hiyo ndiyo Sauti itakayomunganisha na kumkamilisha Bibi-Arusi. Ukiyaondoa macho na masikio yako kwenye Sauti, Utatoka mstarini na kuingia katika machafuko matupu.

Kila Ujumbe unakuwa wazi zaidi na zaidi. Ni Mungu aliye mkuu Akifunuliwa mbele zetu, akimlisha Bibi-Arusi Wake Mana Iliyofichwa ndiyo tu tunayoweza kula. Ni nono sana kwa wengine wote, bali ni Chakula Kilichofichwa kwa ajili ya Bibi-Arusi.

Ni wakati wa kutoa Shukrani uliyoje Bibi-arusi alionao, akila Neno, akifanyika Bibi-arusi Neno Wake Mkamilifu.

Anasimama peke yake, kama Bwana Arusi, amekataliwa na watu, amedharauliwa na kukataliwa na makanisa. Bibi-arusi yuko hivyo. Ni nini? Ni Kipeo Chake. Mnaona? Ni Neno Yeye analoweza kutendea kazi kwake na kulidhihirisha, likikataliwa.

Njooni muungane nasi Jumapili saa 6:00 MCHANA, saa za Jeffersonville,(ni saa 2 USIKU ya Afrika Mashariki) Wakati Mungu akizungumza kupitia malaika Wake mwenye nguvu, na kutukata na kutuadibisha ili tufanyike Kipeo cha Mungu.

Ndugu Joseph Branham

Ujumbe: 64-0705 Kile Kipeo

Maandiko ya kusoma kabla ya ibada:
Isaya 53:1-12
Malaki 3:6
Mathayo Mt. 24:24
Marko Mt. 9:7
Yohana Mt. 12:24 / 14:19

25-1123 Mungu Aliye Mkuu Akifunuliwa Mbele Zetu

UJUMBE: 64-0629 Mungu Aliye Mkuu Akifunuliwa Mbele Zetu

PDF

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Maskani Ya Branham,

Tunakuwa na nyakati tukufu jinsi gani. Neno na Bibi-arusi ni Mmoja na jambo lile lile. Tunaishi nyuma ya pazia katika Uwepo wa Utukufu wa Shekina. Tunamwona Mungu akijificha nyuma ya ngozi katika malaika-mjumbe Wake wa saba. Mungu, kwa mara nyingine tena, akijificha nyuma ya ngozi ya mwanadamu katika kila mmoja wetu. Hakuna swali tena. Hakuna shaka tena, sisi NDIYO wateule Wake, waliochaguliwa tangu zamani, Neno lililofanyika mwili, Bibi-arusi Neno mkamilifu.

Tunapoungana pamoja kutoka kote ulimwenguni, tunaisikiliza Sauti Yake ikinena na kutufunulia Neno Lake kikamilifu ule Ufunuo mkamilifu kwamba Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele. Dhihirisho la Neno, Elohim, Mungu katika mwili akizungumza na Bibi-arusi Wake. Mungu katika mwili akiishi na kukaa ndani ya kila mmoja wetu. Mpango wa mwisho wa Mungu sasa unadhihirishwa kikamilifu na kuonyeshwa ndani ya kila mmoja wetu.

Tunayofuraha kwelikweli na tunamshukuru Bwana sisi kuitwa wa kipekee na nati zenye hesi za mwonekano wa ajabu. Lakini tunajua yule tuliyeingizwa kwake, na sisi ni nani: Bibi-arusi wa Mungu aliyetiwa Hesi kwa Kanda; Nayo inatuvuta Kwake Yeye Mwenyewe, ikizidi kukaza zaidi na zaidi tunapokuwa MMOJA PAMOJA NAYE, Yesu Kristo yeye yule jana, leo, na hata milele.

Tumepenya katika pazia na kuingia katika Nguzo ya Moto nasi tumetoka na baraka za Mungu! Watu hawawezi kuliona. Hawawezi kulielewa. Lakini kwetu sisi, liko wazi kabisa, kwa sababu tuko katika Roho yule yule na Mtunzi wetu na Kiongozi wetu. Ni Sauti ya Mungu iliyo kwenye Kanda ndiyo inayomwongoza Bibi-arusi Wake.

Tunaishi kwa Mkate wa Wonyesho, Mana inayopewa tu watu waliotengwa. Ndicho Kitu pekee tunachoweza kula. Ndicho kitu pekee tunachoruhusiwa kula. Nacho ni kwa ajili tu ya watu wale ambao wameruhusiwa, waliochaguliwa kimbele na wanaojua hicho nini.

Mimi ninapenda tu kumsikia Yeye akituambia SISI NI NANI:

Yeye aliyeshuka katika siku ya Pentekoste ndiye Roho Mtakatifu yule anayedhihirishwa siku hizi, toka utukufu, hata utukufu, hata utukufu, na kurudia ile mbegu yake asili kwa Ubatizo wa Roho Mtakatifu, pamoja na ishara zile zile, ajabu zile zile ubatizo ule ule, watu wa aina ile ile wakitenda vile vile, wakiwa na uweza ule ule, mwamsho ule ule. Ni kutoka utukufu hata utukufu.

Tumerudi kwenye Mbegu asili pamoja na ubatizo wa Roho Mtakatifu. Ishara zile zile, maajabu yale yale, ubatizo ule ule, watu wa aina ile ile, tukitenda vile vile, kwa uweza ule ule, mwamsho ule ule.

SISI NDIYO BIBI-ARUSI NENO WAKE MKAMILIFU WA KANDA, ALIYEREJESHWA KIKAMILIFU!

Tunashinda. Tunabaki. Tunasimama. Tupo kwenye Neno Lake safi ambalo limehifadhiwa kwa ajili ya Bibi-arusi Wake. Linatukamilisha siku baada ya siku. IMANI yetu imefikia viwango vipya tukijua SISI NI NANI, nayo:

Haikanushiki, Haijadiliki na zaidi ya yote, HAINA MASHARTI.

Je, unataka kuwa mwenye furaha zaidi kuliko ulivyowahi kuwa?
Je, unataka kuridhika 1000% kwamba kile unachokisikia ni Bwana Asema Hivi? Je, unataka kukamilishwa na Neno la Mungu?

Basi ninakualika uje uungane nasi, Maskani ya Branham, Jumapili hii saa 6:00 MCHANA, saa za Jeffersonville, (ni saa 2 USIKU ya Afrika Mashariki) tunapoisikia Sauti ya Mungu ikituambia Maneno ya Uzima wa Milele: Mungu Aliye Mkuu Akifunuliwa Mbele Zetu 64-0629.

Ndugu Joseph Branham

25-1116 Kristo Aliyetambulishwa Katika Nyakati Zote

UJUMBE: 64-0617 Kristo Aliyetambulishwa Katika Nyakati Zote

PDF

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Neno La Mungu Lililo Hai,

Miaka hii yote nimelificha moyoni mwangu, nikimficha Kristo, Nguzo ile ile ya Moto ikilifasiri Neno, kama ilivyoahidiwa.

Najua hili litasikika kama la kipuuzi kwa watu wengi, lakini ikiwa tu utamvumilia malaika-mjumbe wa Mungu kwa dakika chache, na kumwomba Mungu Ufunuo zaidi, naamini kwamba yeye, kwa msaada wa Mungu na kwa Neno Lake, na kulingana na Neno Lake, atamleta Yeye hapa mbele yako. Mungu, akijifunua na kujidhihirisha Mwenyewe, akilifasiri na kulifunua Neno Lake.

Ni uamsho ulioje ambao umekuwa ukitendeka mwezi huu uliopita ndani ya Bibi-arusi wa Yesu Kristo. Mungu, akijifunua Mwenyewe zaidi ya wakati wowote ule, akizungumza na Kipenzi Chake, akifanya mapenzi Naye, akimhakikishia, Sisi ni Mmoja na Yeye.

Hakuna kusitasita, hakuna kutokuwa na uhakika, hakuna kushuku, hakuna shaka hata chembe; Mungu ametufunulia: Sauti ya Mungu inayozungumza kwenye kanda ndio NJIA YA MUNGU ILIYOANDALIWA NA ILIYOKAMILIFU KWA BIBI-ARUSI WAKE LEO.

Aliiandaa njia hii ili Tusije kamwe tukalazimika hilo kuwekewa chujio, kufafanuliwa, kuelezewa, wala kushikwa-shikwa na mikono ya watu kwa njia yoyote; kuisikiliza tu Sauti Safi ya Mungu ikizungumza mdomo kwa sikio na kila mmoja wetu.

Yeye alijua siku hii ilikuwa inakuja. Alijua Bibi-arusi Wake angeweza kula tu hiyo Mana iliyofichwa, Chakula Chake cha Kondoo. Hatungetaka kusikia chochote ila Sauti ya Mungu kutoka kwa Mungu Mwenyewe.

Tumevunja tukapitia kwenye pazia hilo nasi tumeingia katika Utukufu wa Shekina. Ulimwengu hauwezi kuliona. Nabii wetu huenda asiyatamke maneno yake ipasavyo. Huenda asivalie ipasavyo. Huenda asivikwe mavazi ya kikasisi. Lakini nyuma ya ngozi hiyo ya kibinadamu, mle ndani mna ule Utukufu wa Shekina. Mle ndani mna nguvu. Mle ndani mna Neno. Mle ndani mna Mkate wa Wonyesho. Mle ndani mna Utukufu wa Shekina, ambao ndiyo Nuru inayomwivisha Bibi-arusi.

Na mpaka utakapokuja nyuma ya hiyo ngozi ya pomboo, mpaka utakapotoka nyuma ya ngozi yako ya kale, mawazo yako ya kale, kanuni zako za imani za kale, na uingie katika Uwepo wa Mungu; ndipo Neno linakuwa hali halisi iliyo hai kwako, ndipo umeinuka katika Utukufu wa Shekina, ndipo Biblia inakuwa ni Kitabu Kipya, ndipo Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo, na hata milele. Unaishi katika Uwepo Wake, ukila mkate wa wonyesho ambao unatolewa tu siku hiyo kwa waaminio, makuhani pekee. “Na sisi ni makuhani, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa kipekee, tukimtolea Mungu dhabihu za kiroho.” Lakini huna budi kuingia, huko nyuma ya pazia, upate kumwona Mungu aliyefunuliwa. Na Mungu anafunuliwa, hilo ni Neno Lake lililodhihirishwa.

Sisi ni wa kipekee kwa ulimwengu, lakini tumeridhika kujua Skrubu yetu ni nani na tunajivunia sisi kuwa nati Zake za kanda, tuliyotiwa hesi kwa Neno Lake, kwani linatuvuta Kwake.

Kama hujaingizwa kwenye kanda, wewe si kitu ila lundo la vitu shaghalabaghala!!!

Sasa, angalieni sasa, Mungu! Yesu alisema ya kwamba, “Wale waliojiliwa na Neno, waliitwa ‘miungu,’” hao walikuwa ni manabii. Sasa, si kwamba mtu huyo mwenyewe alikuwa ni Mungu, si zaidi ya vile mwili wa Yesu Kristo ulivyokuwa ni Mungu. Yeye alikuwa ni mwanadamu, Naye Mungu alikuwa amefunikwa nyuma yake.

Mungu, siku moja alifunikwa nyuma ya ngozi za pomboo. Mungu, siku moja alifunikwa katika mwili wa mwanadamu aitwaye Melkizedeki. Mungu, alifunikwa katika mwili wa mwanadamu aitwaye Yesu. Mungu, alifunikwa katika mwili wa mwanadamu aitwaye William Marrion Branham. Mungu, amefunikwa katika mwili wa mwanadamu aitwaye BIBI-ARUSI WAKE.

Ni muhimu sana kukumbuka, lakini walio wengi wanashindwa na wanatafuta kitu kingine. Jambo la mwisho ambalo Ibrahimu aliona, jambo la mwisho kutukia kabla ya moto kushuka na kuuhukumu ulimwengu wa Mataifa, kabla ya yule mwana aliyeahidiwa kutokea, jambo la mwisho ambalo kanisa la Kikristo litaliona mpaka kule kuonekana kwa Yesu Kristo ni Melkizedeki, Mungu aliyedhihirishwa katika mwili, akilifunua Neno Lake kwa Bibi-arusi Wake.

Hakuna kitu kingine kitakachokuja. Hakuna kitu kingine kilichoahidiwa katika Neno Lake. Hakuna mtu, wala kundi la watu watakaokuja kumkamilisha Bibi-arusi.

La! Wanataka kuja humu kanisani kwa ajili ya kukamilishwa. Ona? Ili sisi—sisi tupate ushirika sisi kwa sisi hapa kanisani, lakini kukamilishwa huja kati yetu na Mungu. Damu ya Kristo ndiyo inayotukamilisha katika Roho Mtakatifu.

Ujumbe huu, Sauti Hii, Neno la Mungu lililothibitishwa, linamkamilisha Bibi-arusi wa Yesu Kristo.

Ninawaalika kila mmoja wenu mje muisikilize pamoja nasi Sauti ya Mungu inapomkamilisha Bibi-arusi Wake Jumapili hii saa 06:00 MCHANA, saa za Jeffersonville,(ni saa 2 USIKU ya Afrika Mashariki) tunaposikia: 64-0617 “Kristo Aliyetambulishwa Katika Nyakati Zote”.

Ndugu. Joseph Branham

Maandiko ya kusoma kabla ya Ujumbe:
Kumbukumbu la Torati 18:15
Zekaria 14:6
Malaki 3: 1-6
Luka Mtakatifu 17: 28-30
Yohana Mtakatifu 1:1 / 4:1-30 / 8: 57-58 / 10:32-39
Waebrania 1:1 / 4:12 / 13:8
Ufunuo 22:19

25-1109 Wa Kipekee

UJUMBE: 64-0614E Wa Kipekee

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Mungu Aliye Na Ngozi,

Hatuko nyuma ya pazia tena, enyi watoto wadogo, Mungu ameonekana wazi kwetu. Yule Mungu mkuu wa Mbingu na nchi, ambaye daima amejificha Mwenyewe kwa watu kama Nguzo ya Moto ile iliyotoka kwa Mungu na kuishi katika mwili wa duniani unaoitwa Yesu; kisha akarudi kwenye ile Nguzo ya Moto na akamtokea Paulo njiani akielekea Dameski, sasa ameonekana tena wazi kabisa na akakaa tena katika mwili wa mwanadamu ndani ya malaika-Mjumbe Wake, William Marrion Branham, akimwita Bibi-arusi Wake atoke aende Kwake.

Mungu alimweka malaika Wake duniani kujiwakilisha Mwenyewe kama balozi Wake aliyechaguliwa kuingia katika mambo makuu yasiojulikana ya kimbinguni. Yeye anatambua na kuyaleta mambo ambayo akili ya kawaida haiwezi kuyaelewa. Alitumwa kuweka wazi siri ya Mungu na kutabiri mambo yaliyopo, na mambo ambayo yamekuwepo, na mambo ambayo yatakuwepo. Yeye ni Sauti ya Mungu kwa Bibi-arusi.

Ni nini? Mungu, Mungu nyuma ya ngozi, ngozi ya binadamu. Kweli hasa.

Watoa lawama wengi leo hawawezi kutuelewa sisi waaminio wa kweli. Kwao, sisi tumekuwa nati. Wanasema ati sisi ni waamini mungu-mtu tunamwabudu nabii…

Mtoa lawama, siku chache zilizopita, aliniambia, kule chini Tucson. Alisema, “Unajua, watu wengine hukufanya wewe nati, na wengine wanakufanya mungu.”
Nikasema, “Vema, jambo hilo liko sawa kwa namna fulani.” Nilijua anajaribu kunilaumu. Mnaona?
Yeye akasema, “Watu wanafikiri wewe ni mungu.”

Kama jinsi ilivyokuwa wakati Yesu alipokuwa hapa duniani, ni vivyo hivyo leo hii kwa nabii Wake. Watu hawako nyuma ya pazia; wao wamepofushwa kuihusu kweli. Sisi hatutaki lolote ila njia ya Mungu iliyoandaliwa kwa ajili ya siku hii: Yeye Mwenyewe akiwa amefunikwa katika mwili, Sauti ya Mungu iliyorekodiwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya Bibi-arusi.

Mungu alipodhihirishwa ulimwenguni, Yeye alikuwa amejificha nyuma ya pazia, nyuma ya ngozi ya Mtu aliyeitwa Yesu. Yeye alikuwa ametiwa utaji na kujificha nyuma ya ngozi ya mtu aliyeitwa Musa, nao walikuwa miungu, si Mungu; bali walikuwa Mungu, yule Mungu mmoja, akibadilisha kinyago Chake tu, akifanya jambo lile lile kila wakati, akileta Neno hili. Mungu alilifanya jinsi hiyo.

Tumeingizwa tu na Neno, Ujumbe wa saa hii. Sasa imetufanya kuwa Neno lililofichwa nyuma ya mwili wa mwanadamu. Bibi-arusi na Bwana-arusi ni mmoja. Mungu ni mmoja, nalo Neno ni Mungu! Tumetiwa hesi kwa Neno.

La kusikitisha, utengano miongoni mwa waaminio leo ni kwamba wao wanahisi tunamtukuza sana nabii wa Mungu aliyethibitishwa. Kinyume chake, wao wanataka kuuweka uongozi huo juu ya wachungaji wao.

Mungu Yeye habadilishi mpango Wake; Anamtuma MTU MMOJA kumwongoza Bibi-arusi Wake. Ni Roho Wake Mtakatifu ndani ya kila mmoja wetu, akituongoza kwa NGUZO YA MOTO.

Neno humjia mmoja. Katika kila wakati, vivyo hivyo, hata katika nyakati za kanisa, tangu wa kwanza hadi wa mwisho. Wengine wana mahali pao, hiyo ni kweli, angalia, lakini kaeni mbali na hiyo Nguzo ya Moto. Unaona?

LAKINI TUNASIKIA NINI LEO…JAMBO LILE LILE.

Mnakumbuka yale Dathani na hao wengine waliyosema kule njiani? Walisema, “Sasa, Musa, hebu ngoja hapa kidogo tu! Unajitukuza sana, unaona. Sasa, wapo watu wengine hapa ambao Mungu amewaita.”

Sisi hatuwapingi wahudumu; Mungu amewaita, Lakini Enyi ndugu na dada, ikiwa mchungaji wenu haiweki Sauti ya Mungu Mwenyewe kuwa ndio Sauti iliyo muhimu zaidi mnayopaswa kuisikia kwa kuzicheza kanda kanisani mwenu, yeye hawaongozi kwenye Njia ya Mungu iliyoandaliwa.

Hiyo ni kweli. Wao, kila mmoja, walikuwa wakifuata vizuri mradi tu waliendelea mbele, lakini wakati mmoja alipojaribu kuinuka na kuchukua nafasi ya Mungu ambayo alikuwa amempa Musa, ambaye alikuwa amekusudiwa tangu zamani na kuchaguliwa kwa ajili ya kazi hiyo, alipojaribu kupachukua, moto ulishuka na ukaifunua nchi na kuwameza moja kwa moja ndani yake. Unaona? Unaona? Kuwa mwangalifu. Unaona?

Tunapaswa sote tuingizwe kwenye Neno hilo lililonenwa na kuwekwa kwenye kanda. Hilo ndio Yakini ya Mungu. Hilo ndilo Neno pekee ambalo Bibi-arusi anaweza kukubaliana kwalo. Wahudumu hawataweza kamwe kumuunganisha Bibi-arusi, ni Sauti ya Mungu iliyo kwenye kanda peke yake.

Mimi siwezi kufanya kitu bila ninyi; ninyi hamwezi kufanya kitu bila mimi; hakuna anayeweza kufanya kitu bila Mungu. Kwa hiyo, sote pamoja linafanya kitu kimoja, ule muungano. Mungu alinituma kwa kusudi hilo; mnaamini jambo hilo; na hapa linatendeka. Ndilo hilo hasa, mnaona, limehakikishwa kikamilifu.

Ni kwa pamoja TU ndipo inafanya KITU KIMOJA, ule muungano. Mungu alimtuma William Marrion Branham kwa kusudi hilo. Basi, ikiwa TU utaliamini Hilo, Litatendeka; limehakikishwa kikamilifu.

Si mimi ninayelisema hilo, Enyi ndugu na dada. NI MUNGU ANAYELISEMA HILO KUPITIA NABII WAKE. Msimruhusu mtu yeyote awaambieni tofauti ama kujaribu kuwafafanulieni kitofauti. NI SAUTI YA MUNGU ILIYO KWENYE KANDA TU NDIYO ITAKAYOMUUNGANISHA NA KUMKAMILISHA BIBI-ARUSI. KWA NJIA NYINGINE YOYOTE, HUTAKUWA BIBI-ARUSI.

Kwa hiyo nafikiri wengi wetu sisi watu wazima tunafikiria vivyo hivyo. Mungu, aliye na ngozi! Linaweza likasikika kama nati, kwa ulimwengu, bali linawavuta watu wote Kwake.

Mnasikia alichotoka kusema? Mungu aliye na ngozi anawavuta watu wote Kwake.

Wakati ulimwengu umetiwa hesi kwa ajili ya nati, sisi tumetiwa hesi kwa Sauti ya Mungu nasi tunaitwa Bibi-arusi. Inatuvuta kututoa katika mchafuko huu, kutuingiza katika Uwepo wa Mungu. Sisi ni nati tuliyotiwa hesi kwa Neno la Mungu.

Njooni na muingizwe kwenye Sauti ya Mungu pamoja nasi Jumapili hii saa 06:00 MCHANA, saa za Jeffersonville, (ni saa 2:00 USIKU ya Afrika Mashariki) huku Ikiwavuta watu wote Kwake.

Ndugu Joseph Branham

Ujumbe: Wa Kipekee. 64-0614E

Maandiko:

1 Wakorintho 1:18-25
2 Wakorintho 12:11

25-1102 Kufunuliwa Kwa Mungu

UJUMBE: 64-0614M Kufunuliwa Kwa Mungu

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Neno Lililodhihirishwa,

Je, tunaweza kuliwazia hilo! Nguzo ile ile ya Moto iliyowajia wale watu walioiandika Biblia ndio nguzo ile ile ya Moto tunayoisikia kila siku, ikitufasiria siri zote za Biblia: Neno la Mungu lililodhihirishwa!

Mungu alikuwa amejifunika katika manabii Wake ili aweze kuyanena maneno Yake, hilo ndilo Yeye alilolifanya wakati huo, lakini katika siku yetu, William Marrion Branham, Yeye alikuwa ndiye Neno lililo Hai kwa watu, lililofunikwa kwa Nguzo ya Moto.

Ule upako ni mtu. Neno Kristo maana yake ni aliyetiwa mafuta, mnaona, “aliyetiwa mafuta.” Basi, Musa alikuwa ni Kristo katika siku zake, alikuwa ndiye mtiwa mafuta. Yeremia alikuwa ni Kristo katika siku zake, akiwa na sehemu ya Neno kwa siku hizo.

Mungu hujifasiria Neno Lake Mwenyewe; Mungu alilifasiri, Yeye ndiye aliyekuwa na Neno, si kundi, bali William Marrion Branham!

Mungu alimchukua mtu MMOJA, Yeye hawezi kuwachukua watu wawili ama watatu wenye mawazo tofauti, Yeye humchukua mtu MMOJA, naye akawa Neno lililo Hai lililofunuliwa nyuma ya mwili wa mwanadamu.

Hatuko nyuma ya pazia hilo tena, enyi Watoto wadogo. Mungu anaonekana wazi kabisa kwetu. Ule utaji wa kale wa kimadhehebu na wa mapokeo umepasuliwa kutoka kwenye Neno la Mungu, kusudi lipate kudhihirishwa! Katika siku hii ya mwisho, ule utaji wa mapokeo umepasuliwa, na hii hapa imesimama Nguzo Ya Moto. Huyu hapa, akidhihirisha Neno kwa ajili ya siku hii. Pazia limepasuliwa.

Tazameni hizo kanda zinavyofuatana, tazameni kila moja, jinsi imekuja ikiwa dhahiri zaidi na zaidi; kama mna masikio ya kusikia, mnaona, macho ya kuona.

Hilo ndilo linalowapofusha watu leo, wao wanataka kusema kuwa nabii wa Mungu ndiye aliyelileta Neno, Lakini hivi sasa huo upako upo juu ya wengine ili kutuongoza, sio nabii.

Nabii alituambia kuwa Mungu hawezi kulivunja Neno Lake, katika siku za mwisho haina budi kuwa ni jambo lile lile tena, Mungu hawezi kuibadilisha Njia Yake, ama kulibadilisha Neno Lake, Yeye alisema habadiliki. Yeye aliwatuma manabii Wake sio tu kulileta Neno Lake bali kumwongoza Bibi-arusi Wake.

Kama ilivyofanyika katika kila wakati, Uungu ukitiwa utaji katika mwili wa binadamu. Angalieni, Yeye alifanya hivyo. Manabii walikuwa ni Uungu, umetiwa utaji. Walikuwa ni Neno la Mungu (hiyo ni kweli?) lililotiwa utaji katika mwili wa binadamu. Kwa hiyo wala hawakumwona Musa wetu, mnaona, Yesu.

Sasa si Neno tu lililoandikwa kwetu, ni kitu halisi. Tuko ndani Yake. Sasa tunafurahia. Sasa tunamwona Yeye. Sasa tunamwona, lile Neno, akijidhihirisha Mwenyewe.

Ndipo tunakuwa sehemu Yake, utaji unaomficha Yeye. Sisi ni sehemu Yake; mradi Kristo yumo ndani yetu, kama vile Kristo alivyokuwa wa Mungu, sisi tunamfunika Kristo katika hekalu letu la ngozi ya kibinadamu. Sisi ni nyaraka zilizoandikwa. Neno lililoandikwa. Sisi ni Neno lililoandikwa lililodhihirishwa.

Na mnapoliona Neno likidhihirishwa, mnamwona Baba, Mungu, kwa kuwa Neno ni Baba. Neno ni Mungu. Nalo Neno, likidhihirishwa, ni Mungu Mwenyewe akichukua Neno Lake Mwenyewe na kulidhihirisha miongoni mwa waaminio. Hakuna kitu kinachoweza kulifanya liishi ila waaminio, waaminio tu.

Mungu, amefunikwa katika mwili wa mwanadamu, akinena na kutufunulia Neno Lake siku baada ya siku. Mungu katika mwili wa mwanadamu akiishi ndani ya kila mmoja wetu.

Ndugu Joseph Branham

Ujumbe:
(64-0614m Kufunuliwa Kwa Mungu.)

Muda: saa 6:00 MCHANA saa za Jeffersonville( ni saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki ).

Kumbukeni masaa ya kukomboa nyakati za mchana

25-1026 Tazama Aliko Yesu

UJUMBE: 63-1229E Tazama Aliko Yesu

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Wapendwa Wasikilizaji Wa Kanda,

Wakati umefika ambapo kila mtu lazima ajiulize mwenyewe: “Ninapozisikiliza kanda, ni Sauti gani ninayoisikia? Je! ni sauti ya William Marrion Branham tu, au ninaisikia Sauti ya Mungu ya siku yetu? Je! ni neno la mwanadamu, au ninaisikia Bwana Asema Hivi? Je! ninamhitaji mtu fulani wa kunifasiria kile ninachokisikia, au Neno la Mungu halihitaji fasiri yoyote?”

Jibu letu ni: Tunasikiliza Neno Lililonenwa lililofanyika mwili. Tunamsikiliza Alfa na Omega. Tunamsikiliza Yeye, ile Nguzo ya Moto, akizungumza kupitia midomo ya mwanadamu kama alivyosema angefanya katika siku yetu.

Sisi hatumsikii mwanadamu, tunamsikia Mungu, yeye yule jana, leo, na hata milele. Sauti ya Mungu iliyo hai, yenye nguvu kuliko upanga ukatao kuwili, yenye kukata hata kuugawanya mfupa, na kuyatambua mawazo yaliyo moyoni.

Imefunuliwa kwetu ya kwamba kile Yeye alichokuwa wakati alipotembea Galilaya ni jambo lile lile alilo usiku wa leo huku Jeffersonville; jambo lile lile Yeye alilo kwenye Maskani ya Branham. Ni Neno la Mungu likidhihirishwa. Kile alichokuwa wakati huo, ndicho alicho usiku wa leo, na atakuwa hivyo milele. Kile alichosema angefanya, amekifanya.

Mtu huyo si Mungu, lakini Mungu angali anaishi na kuzungumza na Bibi-arusi Wake kupitia mtu huyo. Sisi hatuthubutu kumwabudu mtu huyo, bali tunamwabudu Mungu aliye katika mtu huyo; kwa maana yeye ndiye mtu ambaye Mungu alimchagua kuwa SAUTI YAKE na kumwongoza Bibi-arusi Wake katika siku hizi za mwisho.

Kwa sababu Yeye ametupa Ufunuo huu mkuu wa wakati wa mwisho, tunaweza sasa kujitambua SISI NI NANI, Neno lililofanyika mwili katika siku yetu. Shetani hawezi tena kutulaghai, kwa maana tunajua sisi ni Bibi-arusi Neno bikira Wake aliyerejeshwa kikamilifu.

Sauti hiyo ilituambia: Yote tunayohitaji TAYARI tulikwishapewa. Hakuna haja ya kusubiri. Lilishanenwa, NI YETU, NI MALI YETU. Shetani hana uwezo juu yetu; ameshindwa.

Hakika, Shetani anaweza kututupia magonjwa, huzuni, na maumivu ya moyo, lakini Baba Yeye tayari amekwisha kutupa uwezo wa kumfukuza ATOKE…TUNANENA NENO TU, naye hana budi kuondoka….si kwa Sababu sisi tunasema hivyo, bali kwa sababu MUNGU ALISEMA HIVYO.

Mungu yeye yule aliyewaumba kindi, wakati hapakuwa na kindi. Yule aliyempa Dada Hattie haja ya moyo wake: wanawe wawili. Yule aliyemponya Dada Branham uvimbe kabla ya mkono wa daktari haujamgusa. Yeye ni MUNGU YULE YULE ambaye si tu kwamba yuko pamoja nasi, BALI ANAISHI NA KUKAA NDANI YETU. SISI NI NENO LILILOFANYIKA MWILI.

Tunapotazama na kusikiliza Sauti iliyo kwenye kanda, tunaona na kumsikia Mungu akijifunua katika mwili wa mwanadamu. Tunaona na kusikia ni nani aliyetumwa na Mungu kutuongoza kwenda kwenye Nchi ya Ahadi. Tunatambua ni Bibi-arusi peke yake ndiye atakayekuwa na Ufunuo huo, kwa hiyo tumekuwa tusioogopa. Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi, kufadhaika, kuchanganikiwa, kushangaa au kuhofu…SISI NDIO BIBI-ARUSI.

Sikiliza uishi, ndugu yangu, ishi!
Msikilize Yesu sasa upate kuishi;
Kwa maana Imerekodiwa kwenye kanda, haleluya!
Ni kwamba tu tusikilize tupate kuishi.

Loo, Bibi-arusi wa Yesu Kristo, ni siku iliyo kuu jinsi gani tunayoishi. Tunayongojea, dakika baada ya dakika. Siku yoyote tu sasa tutawaona wapendwa wetu, kisha, katika dakika moja, kufumba na kufumbua jicho, tutaondoka mahali hapa na pamoja nao ng’ambo ya pili. Hilo liko karibu sana yaonekana tunaweza kulihisi…UTUKUFU!

Njooni enyi Bibi-arusi, hebu na tuungane kwa mara nyingine tena kwenye Sauti ya Mungu Jumapili hii saa 06:00 MCHANA, saa za Jeffersonville,(Ni saa 1 JIONI ya Afrika Mashariki) tunapomsikia Yeye akizungumza nasi Neno la Uzima wa Milele.

Ndugu. Joseph Branham

Ujumbe: 63-1229E Tazama Aliko Yesu

Maandiko:
Hesabu 21:5-19
Isaya 45:22
Zekaria 12:10
Yohana 14:12

25-1019 Yupo Mtu Hapa Anayeweza Kuiwasha Taa

UJUMBE: 63-1229M Yupo Mtu Hapa Anayeweza Kuiwasha Taa

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Bibi-arusi wa Kristo, hebu na tukutane pamoja Jumapili saa 06:00 MCHANA, saa za Jeffersonville,(ni saa 1:00 JIONI ya Afrika Mashariki) ili kusikia 63-1229M Yupo Mtu Hapa Anayeweza Kuiwasha Taa.

Ndugu. Joseph Branham

25-1012 Kukata Tamaa

UJUMBE: 63-0901E Kukata Tamaa

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Bibi-arusi Wa Kanda,

Sasa, ninyi watu kwenye kanda.

Bwana, tunawezaje kuanza kueleza kile maneno haya madogo sita yanachomaanisha kwetu sisi, Bibi-arusi wa Yesu Kristo? Ndio Ufunuo wa Ujumbe wa saa hii kwetu sisi. Ni Mungu akizungumza kupitia malaika-mjumbe Wake akimwambia Bibi-arusi Wake, “Ninajua mtadumu na Sauti Yangu. Ninajua Neno Langu lililo kwenye kanda hizi vile litakavyomaanisha kwenu. Ninajua mtakuwa na Ufunuo ya kwamba Jumbe hizi nilizozinena kwenye kanda ndio Ishara Yangu ya wakati huu.”

“Nimeiweka Sauti Yangu kwenye kanda hizi za sumaku; kwa maana Jumbe hizi hazina budi kulimalizia Neno lote. Kutakuwako na maelfu mara maelfu ambao wataisikia Sauti Yangu kwenye kanda nao watakuwa na Ufunuo ya kwamba hii ndiyo huduma Yangu. Ndio Roho Mtakatifu wa wakati huu. Ndio Ujumbe Wangu ulio Ishara”

“Nimewatuma wahudumu wengi waaminifu ulimwenguni kote kuitangaza huduma Yangu. Waliporudi, waliniambia, ‘Tumeyatii maagizo Yako kwa kuzicheza kanda Zako. Tumewapata watu walioamini kila Neno. Wamezifanya nyumba zao wenyewe kuwa kanisa kuupokea Ujumbe Wako. Tuliwaambia, wote ambao wangekuja chini ya Ishara Yako, Ujumbe wa saa hii, wangeokolewa.’”

Ni wakati ambapo kila mtu lazima ajichunguze na kujiuliza, Ni ipi njia kamilifu ya Mungu ya siku hii? Neno la nabii halijashindwa hata wakati mmoja. Limethibitishwa kuwa ndiyo Kweli PEKEE, ndicho kitu PEKEE kitakachomuunganisha Bibi-arusi Wake.

Chochote yeye alichokisema kimetukia jinsi vile hasa alivyokisema. Nguzo ya Moto ingali hapa pamoja nasi. Sauti ya Mungu ingali inazungumza nasi kwenye kanda. Nabii amemaliza kutuambia ya kwamba Mungu angepita juu wakati tu atakapoiona ile Ishara. Ni wakati wa kudhikika kwa wote kuingia chini ya Ujumbe huo ulio Ishara.

Tumeuona Mkono mkuu wa Mungu katika wakati huu wa mwisho. Ametupa Ufunuo wa kweli wa Neno Lake nao umekuja chini ya ushahidi wa ile Ishara. Sasa, wakati tuwapo chini ya ushahidi wa ile Ishara, hebu na tukusanyike pamoja na kuula Ushirika kwa kudhikika; kwa maana tunajua kwamba Mungu yuko tayari kutoa hukumu.

Ningependa kuwaalika kila mmoja wenu kusikia na kuwa na Ibada ya Ushirika na Kutawadhana Miguu Miguu Jumapili hii, tunapousikia Ujumbe: Kukata Tamaa 63-0901E.

Ujumbe na Ibada ya Ushirika itakuwa kwenye Redio ya Sauti kuanzia saa 11:00 JIONI. Saa za Jeffersonville. Tafadhali jisikieni huru kuifanya ibada yenu saa 11:00 JIONI. Kwa masaa ya maeneo yenu mkipenda, kama nijuavyo itakuwa vigumu kwa waamini wetu wengi wa nchi za ng’ambo kuianza ibada yenu kwa wakati huo wa huku. Kutakuwa na anuani ya faili la kupakuliwa la ibada.

Ndugu. Joseph Branham

Maandiko ya kusoma kabla ya ibada:

Kutoka 12:11
Yeremia 29:10-14
Luka 16:16
Yohana 14:23
Wagalatia 5:6
Yakobo 5:16

25-1005 Ile Ishara

UJUMBE: 63-0901M Ile Ishara

PDF

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Bibi-arusi Wa Ile Ishara,

Tunapokutana pamoja, hatuzungumzi tu juu ya Ujumbe, tunakutana pamoja kuipaka ile Damu, kuiweka ile Ishara; nayo ile Ishara ni Ujumbe wa wakati huu! Huo ndio Ujumbe wa majira haya! Huo ndio Ujumbe wa wakati huu.

Tumeiweka hiyo Ishara kwetu sisi wenyewe, kwa nyumba zetu, na kwa familia zetu. Hatuonei haya. Hatujali nani anayeijua. Tunataka kila mtu aijue, kila mpita njia aione na ajue: Sisi ni Watu wa Kanda. Sisi ni Nyumba ya Kanda. Sisi ni Bibi-arusi wa Kanda wa Mungu.

Roho Mtakatifu = Ile Ishara = Ujumbe. Yote ni mamoja. Huwezi kuyatenganisha. Baba, Mwana, Roho Mtakatifu = Bwana Yesu Kristo. Huwezi kuwatenganisha.

Ujumbe = Mjumbe. Haidhuru wakosoaji wanasema nini, NABII ALISEMA, huwezi kuwatenganisha.

Mungu ndiye furaha yako. Mungu ndiye nguvu zako. Kuujua Ujumbe huu, Kujua ndio Kweli pekee, tukijua ndio ile Ishara, huo ndio utoshelevu wetu. Wengine waweza kusema, “Ninauamini, ninauamini, ninauamini kuwa ni Kweli. Ninaukubali kama Kweli.” Hayo yote ni mazuri, lakini hata hivyo haina budi kuwekwa.

Nabii alisema Ujumbe huu ndiyo ile Ishara ya wakati huu. Ujumbe huu ni Roho Mtakatifu. Kama unao Ufunuo wowote wa Ujumbe huu unaweza kuona waziwazi saa tunayoishi. Wengi sana wanasema, “Ninauamini. Mungu alimtuma nabii. Ni Ujumbe wa wakati huu,” lakini wao wanajigamba kwa kusema hawaichezi, na hawataicheza, Sauti yenyewe ya ile Ishara katika makanisa yao.

Mungu hakunena kupitia malaika Wake mwenye nguvu na kusema tu jambo fulani isipokuwa lilikuwa na maana. Alituambia yeye alitufundisha kwa mifano na vivuli. Katika Ujumbe huu, nabii anaeleza kwa kina sana kutuambia kile Rahabu na familia yake walichofanya ili WAOKOLEWE, kuwa Bibi-arusi. Alikuwa wazi juu ya kile yeye alichofanya.

Wakati wavulana wa kanda walipocheza “KANDA”…Hebu kidogo, mjumbe huyo alifanya nini? Alicheza Kanda. Kisha Rahabu akafanya nini? Aliifanya nyumba yake kuwa KANISA LA KANDA. Hakuonea haya kusema, “Mnaiona ile kamba nyekundu, hiyo inamaanisha kwamba mimi ni KANISA LA KANDA”.

Unadhani kama angalisema, “Ndiyo, ninamwamini mjumbe na Ujumbe, lakini sisi hatuzichezi Kanda tena kanisani mwetu. Ninaye mchungaji anayesema HAPANA, yeye anapaswa tu kuhubiri na kuyanukuu yale Kanda zinachosema.” Hivi unafikiri angeokolewa…???

Akaweka ile ishara, nayo nyumba yake ikaokolewa, ama angaliangamia kule chini alikokuwa.

Umewasikia wahudumu wengi wakitoa visingizio kuhusu kuzicheza kanda, lakini wengi wao husema: “Nabii hakusema kamwe kuzicheza kanda kanisani.”

Nabii alisema Rahabu aliifanya nyumba yake kuwa kanisa, nalo kanisa lake lilizicheza Kanda. Na kwa sababu alizicheza Kanda kanisani mwake, yeye, na Kanisa lake lote la KANDA, walikuwa chini ya ile Ishara na wakaokolewa. Kila kanisa lingine liliangamia.

Ndugu na dada, tafadhali, sisemi mchungaji hawezi kuuhubiri Ujumbe huu, au ni makosa kama anahubiri. Kwa njia yangu mwenyewe, ninahubiri sasa hivi kupitia barua hii, lakini ufungue moyo wako na usikilize kile nabii asemacho na kukuonya. Kama mchungaji wako hachezi, au hatazicheza, kanda kanisani mwenu kwa kutoa udhuru fulani; chochote kile, kulingana na Neno, haidhuru anasema vipi, ninauamini Ujumbe wa wakati huu, kulingana na kile ninachoamini Neno lisemavyo, ile Ishara, Ujumbe wa saa hii, haijawekwa.

Jumapili hii, ninawaalika mje msikilize pamoja na Maskani ya Branham saa 06:00 MCHANA, saa za Jeffersonville,(ni saa 1:00 JIONI ya Afrika Mashariki) Ujumbe: Ile Ishara 63-0901M. Ikiwa hamwezi kuungana nasi, chezeni Ujumbe wowote wa Ile Ishara, na muiweke.

Ndugu. Joseph Branham

Maandiko ya kusoma kabla ya kusikiliza Ujumbe:

Mwanzo 4:10
Kutoka sura ya 12
Yoshua sura ya 12
Matendo 16:31 / 19:1-7
Warumi 8:1
1 Wakorintho 12:13
Waefeso 2:12 / 4:30
Waebrania 6:4 / 9:11-14 / 10:26-29 / 11:37 / 12:24 / 13:8, 10-20
Yohana 14:12

25-0928 Wakati Wa Kuungana Na Ishara Yake

UJUMBE: 63-0818 Wakati Wa Kuungana Na Ishara Yake

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Bibi-arusi Aliyeungana,

Nimechangamshwa sana, na niko chini ya matarajio makubwa ya aina yake, kuwa sehemu ya yote Mungu anayofanya katika siku yetu.  Mawazo ya Mungu ya huko mwanzo sasa yanatimizwa mbele ya macho yetu, na sisi tu sehemu ya hilo.

Kote katika Biblia, manabii walitabiri na kunena yale ambayo yangetukia.  Wakati fulani unabii huo haukutimia kwa mamia ya miaka baadaye, lakini wakati utimilifu wa wakati ulipowadia, ulitimia;  kwa maana mawazo ya Mungu yaliyonenwa kwa kinywa cha nabii Wake LAZIMA yatimie.

Nabii Isaya alisema, “Bikira atachukua mimba”.  Kila familia ya Kiebrania ilimtayarisha binti yao mdogo kumpata mtoto huyu.  Walinunua viatu na vibuti, na nguo ndogo za kichanga, nao wakajitayarisha kwa ajili ya mtoto huyo kuwasili.  Vizazi vilipita, lakini hatimaye Neno la Mungu lilitimia.

Nilipokuwa mvulana mdogo nilishangaa daima, Bwana, naona katika Neno Lako kwamba Wewe daima umewaunganisha watu Wako pamoja ili kulitimiza Neno Lako.  Uliwaunganisha watoto Wako wa Kiebrania kupitia mtu mmoja, Musa, ambaye aliwaongoza kwa Nguzo ya Moto kwenda Nchi ya Ahadi.

Ulipofanyika mwili na kukaa hapa duniani, Wewe uliwaunganisha wanafunzi Wako.  Uliwatenga na kila kitu na kila mtu ili uwafunulie Neno Lako.  Siku ya Pentekoste, kwa mara nyingine tena ulilikusanya Kanisa Lako mahali pamoja, kwa nia moja kwa umoja kabla hujaja na kuwapa Roho Wako Mtakatifu.

Nikawaza, hilo litawezekanaje leo Bwana?  Bibi-arusi Wako ametawanyika kote ulimwenguni.  Je! Bibi-arusi wote watakuja Jeffersonville?  Sijaona hilo likitendeka Bwana.  Lakini BWANA, Wewe kamwe haubadilishi mpango Wako.  Ni Sheria Yako, hakuna njia ya kulizuia hilo.  Utalifanyaje?

UTUKUFU…LEO, tunaweza kuona kwa macho yetu wenyewe, na muhimu zaidi, KUWA SEHEMU YAKE: Neno la Milele la Mungu likitimizwa.  HATUKO KIMWILI mahali pamoja, tumetawanyika ulimwenguni kote, lakini Roho Mtakatifu SASA AMEMUUNGANISHA BIBI-ARUSI WAKE KWA SAUTI YA MUNGU.  NENO LAKE LILILONENWA NA KUREKODIWA KWENYE KANDA, Yakini ya Mungu ya siku hii, inamkusanya na KUMUUNGANISHA BIBI-ARUSI WAKE… NA HAKUNA LOLOTE LINALOWEZA KULIZUIA HILO.

Mungu anamuunganisha Bibi-arusi Wake. Anakusanyika pamoja, kutoka Mashariki na Magharibi, na Kaskazini na Kusini. Kuna wakati wa kuungana, na huo unaendelea sasa hivi. Anaungana kwa sababu gani? Unyakuo. Amina!

Wakati wa kuungana unafanyika SASA HIVI!!!   Ni kitu gani kinachotuunganisha?  Roho Mtakatifu kwa Neno Lake, Sauti Yake.  Tunaungana kwa sababu gani?  UNYAKUO!!!  Nasi tunakwenda sote na hatuachi hata MMOJA nyuma.

Mungu anamtayarisha. Naam bwana, kuungana! Anaungana na kitu gani? Na Neno!

Neno la siku yetu ni lipi?  UJUMBE Huu, SAUTI YAKE, Sauti ya Mungu kwa Bibi-arusi Wake.  Sio mtu.  Sio watu.   Sio kundi. Ni SAUTI ya Mungu iliyo kwenye kanda Iliyothibitishwa, kwa Nguzo ya Moto.

“Kwa maana mbingu zote na nchi zitapita, bali Neno Langu halitapita kamwe.” Anajiunganisha Mwenyewe na BWANA ASEMA HIVI haidhuru madhehebu yoyote ama mtu yeyote mwingine anasema nini.

Haidhuru MTU YEYOTE anasema nini, sisi tunajiunganisha na Sauti ya Bwana Asema Hivi iliyohakikishwa, iliyothibitishwa ya siku yetu.  Sio fasiri ya mtu fulani;  kwa nini tufanye hivyo?  Hiyo hubadilika kwa kila mtu, lakini Sauti ya Mungu iliyo kwenye kanda HAIBADILIKI KAMWE nayo Imetangazwa na Nguzo ya Moto Yenyewe kuwa Neno la Mungu na Sauti ya Mungu.

Shida yake ni kwamba, kwa binadamu, yeye hamjui kiongozi wake. Naam, bwana. Watakusanyika chini ya dhehebu fulani, watakusanyika chini ya askofu ama mtu fulani, bali hawatakusanyika chini ya yule Kiongozi, Roho Mtakatifu katika Neno. Unaona? Wao wanasema, “Loo, vema, nahofu nitakuwa kidogo mshupavu wa dini; ninahofu nitaelekea kubaya.” Loooo, haya basi!

Hapa ndipo wakosoaji wanapoelekezea makutano yao na kusema, “Ona, wanamwinua mtu, Ndugu Branham. Wao ni waabudu mungu-mtu nao wanakusanyika chini yake, mtu huyo, si Roho Mtakatifu.”

Upuuzi, sisi tunaungana chini ya SAUTI YA MUNGU ILIYOTHIBITISHWA ILIYONENWA KUPITIA MTU HUYO.  Kumbukeni, huyo ndiye mtu ambaye Mungu alimchagua kuwa Sauti Yake kumwita atoke na kumwongoza Bibi-arusi Wake katika siku hii.  Hiyo ndiyo Sauti PEKEE iliyothibitishwa na Mungu Mwenyewe.  Lakini kinyume chake, WAO wanaungana chini ya WANADAMU.  HAWATA icheza Sauti ya Mungu iliyo kwenye kanda katika makanisa yao.  Unaweza kuliwazia hilo???  Mhudumu anayedai kuuamini Ujumbe huu kuwa ndio Ujumbe wa wakati huu, Bwana Asema hivi, lakini anatafuta aina fulani ya kisingizio cha KUTO icheza Sauti hiyo makanisani mwao, bali kuwahudumia watu LAZIMA wawasikilize wao na wahudumu wengine wakihubiri Neno… kisha wao wanasema ati sisi tunamfuata mtu!!!

Tumetoka kusikia jumapili iliyopita kile Mungu alichowafanya watu hao!!

Tunajiandaa kufanya Harusi.  Tunafanyika Mmoja na Yeye.  Neno linakuwa wewe, na wewe unakuwa Neno.  Yesu alisema, “Katika siku ile mtaijua. Yote aliyo Baba, ndivyo nilivyo Mimi; na yote niliyo Mimi, ndivyo mlivyo ninyi; na yote mliyo ninyi, ndivyo nilivyo Mimi. Katika siku hiyo mtajua ya kwamba Mimi niko ndani ya Baba Yangu, Baba ndani Yangu, Mimi ndani yenu, nanyi ndani Yangu.”

Asante Bwana kwa Ufunuo wa Wewe Mwenyewe, na wa sisi wenyewe, katika siku yetu.  Bibi-arusi Wako anajiweka mwenyewe tayari kwa Neno Lako Lililonenwa.  Tunajua tuko katika Mapenzi Yako makamilifu kwa sisi kukaa na Neno Lako lililorekodiwa.

Ninaualika ulimwengu kuisikiliza Sauti pekee ya Mungu iliyothibitishwa ya siku yetu Jumapili hii.  Mnakaribishwa muungane nasi Jumapili saa 06:00 MCHANA, saa za Jeffersonville,(ni saa 1:00 JIONI ya Afrika Mashariki) tunaposikia: 63-0818, Wakati Wa Kuungana Na Ishara Yake. Ikiwa hamuwezi kujiunganisha kwa simu na kusikiliza pamoja nasi, chagueni kanda, KANDA YOYOTE;  zote ni Bwana Asema Hivi, na msikilize Neno la Mungu liwakamilishe na kuwafanya tayari kwa ajili ya ujio Wake uliyokaribu.

 Ndugu.  Joseph Branham

 Zaburi 86:1-11
 Mathayo 16:1-3

Anajiunganisha Mwenyewe. Anajitayarisha. Kwa nini? Yeye ni Bibi-arusi. Hiyo ni kweli. Naye amejiunganisha pamoja na Bwana Arusi Wake, unaona, na Bwana Arusi ni Neno. “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili akakaa kwetu.”