Category Archives: Uncategorized

23-1112 Mungu Hamwiti Mtu Hukumuni Bila Ya Kumwonya Kwanza

UJUMBE: 63-0724 Mungu Hamwiti Mtu Hukumuni Bila Ya Kumwonya Kwanza

PDF

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Kamani, Springi kuu, Mkulima na Mke nyumbani,

Chochote kile ambacho Mungu alichokupa kufanya, una utumishi kwa jambo hilo. Huna budi kuwajibika kwa hilo kwa Mungu. Haijalishi adui aweza kukuambia kuwa wewe ni mdogo jinsi gani, wewe ni muhimu sana kwa Mungu hivi kwamba saa Yake kuu haiwezi kusonga bila wewe.

Alikuita, akakuchagua, alikukusudia tangu awali, na akakupa Ufunuo wa Ujumbe Wake mkuu wa wakati wa mwisho. Ana imani na wewe asilimia 100%. Wewe ndiwe yule Bibi-arusi mwenyewe wa Yesu Kristo, Kipenzi Chake, naye Anakupenda sana.

Daima amewaonya watu kote katika mataifa, “Tubuni, la sivyo mtaangamia,” “Rudini kwenye Neno,” “Jitayarisheni, kuna jambo linaenda kutukia.” Wakati huo hatimaye umefika. Mungu anakuja kumchukua Bibi-arusi Wake, kama vile tu alivyotuahidi Angefanya. Ameliita Gurudumu Lake kutoka kwenye gurudumu.

Wengi wameanguka kutoka kwenye Ujumbe mkuu wa Mungu wa wakati wa mwisho leo hii, wakisema, “yale aliyosema yangetukia, hayakufanyika. Mambo yote yako vile vile.” Ilikuwa ni vizazi vingi vilivyopita kabla ya unabii mwingi wa manabii wa Mungu kutimia. Lakini yalitendeka hata hivyo, kama tu walivyosema, Neno kwa Neno.

Biblia yake inatuambia hivi: “Kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika kuja Kwake Mwana wa Adamu.” Kabla Mungu hajatuma hukumu kuuangamiza ule ulimwengu uliotangulia gharika, Mungu alimtuma nabii ulimwenguni. Nabii huyo alifanya nini?

Akawatayarisha watu kwa ajili ya wakati huo. Nuhu aliwatayarisha watu, nao ulikuwa ni wito wa rehema kabla ya hukumu.

Nuhu aliwatayarisha watu kabla ya hukumu kuja aliowaonya kuihusu. Ilikuwa ndio Njia ya Mungu iliyoandaliwa kwa ajili ya siku hiyo.

Nabii wa Mungu alituambia kwamba Mungu kamwe habadilishi mpango Wake. Yale aliyoyafanya wakati huo, anayafanya vivyo hivyo leo hii. Sisi tutakaa tu na MPANGO WA MUNGU ULIYOANDALIWA KWA AJILI YA SIKU HII NA KUBONYEZA PLAY.

Kama ilivyokuwa wakati huo, watu husema tunaweka mkazo sana kwa nabii wa Mungu; Ni Roho Mtakatifu, si William Branham. Tunasema, AMINA, hatumsikilizi huyo mtu , tunasikiliza tu YALE ALIYOSEMA.

Roho Mtakatifu ndiye Nabii wa wakati huu; Yeye analihakikisha Neno Lake, akilithibitisha. Roho Mtakatifu alikuwa ndiye Nabii wa wakati wa Musa. Roho Mtakatifu alikuwa Nabii wa wakati wa Mikaya. Roho Mtakatifu, aliyeliandika Neno, anakuja na kulithibitisha Neno.

Lakini Ndugu Branham ndio kwanza awaambie juma lililopita;

Sasa, mnaona, daima nimewaomba mwe waangalifu kwa yale mnayosikiliza. Mnaona? Kuna mengi sana ambayo ni upande tu wa kibinadamu.

Sisemi ya kwamba Bwana aliniambia jambo hilo. “Mimi” naamini, unaona. Na naamini halipaswi kufanywa.

Kwangu mimi na nyumba yangu, nitachukua yale malaika-mjumbe wa saba wa Mungu ANAYOAMINI, ANAYOWAZIA AU HATA ANAYOJISIKIA kuliko ya mhudumu mwingine yeyote, askofu ama mtu.

Ni nani ambaye Mungu aliwahi kumtuma kuhukumu kile nabii Wake anachoamini, anachohisi ama hata anachofikiria ndicho ama halijavuviwa?…Hebu niwaambieni ni nani ninayefikiri.

Mwangalieni Kora, katika siku ambazo Mungu alimtuma Musa na ujumbe, naye Kora na Dathani wakawazia, wakamwendea Musa, na kusema, “Sasa, hebu kidogo, unajichukulia mengi kupita kiasi! Unafikiri wewe ndiwe changarawe ya pekee ufukoni; bata kidimbwini, ndiwe wa pekee. Nitakufahamisha wapo watu wengine walio watakatifu, pia!”

Onyo, hukumu iko karibu. Rudini kwenye NENO LA ASILI. Rudini kwenye Sauti ya Mungu iliyothibitishwa kwa ajili ya siku yetu. Rudini kwa nabii wa Mungu. Ujumbe huu, Sauti Yake. Inapaswa kuwa ya KWANZA na kuwa jambo lililo muhimu zaidi kwenu.

Bila shaka wengine wana sauti, na wito, kuhubiri na kufundisha Ujumbe huu. Bali Kanda hizo, Sauti hiyo, haina budi kuwa ndio Sauti iliyo muhimu sana mnayopaswa kuisikia katika nyumba zenu, magari yenu, na muhimu zaidi, kanisani mwenu, kama mnataka kuwa Bibi-arusi wa Mungu.

Njooni msikie hiyo Sauti pamoja nasi Jumapili saa 6:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,( ni saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki ) Wakati nabii wa Mungu anapouonya ulimwengu kwamba Kuja kwa Bwana kumekaribia. Hii inaweza kuwa ndio mara ya mwisho.

Ndugu. Joseph Branham

Mungu Hamwiti Mtu Hukumuni Bila Ya Kumwonya Kwanza. 63-0724

Maandiko ya kusoma kabla ya ibada:

Isaya 38:1-5
Amosi Sura ya 1

23-1105 Yeye Hujali. Je! Wewe Unajali?

UJUMBE: 63-0721 Yeye Hujali. Je! Wewe Unajali?

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Wapendwa Watoto wa Injili,

Sisi ni watu waliobarikiwa zaidi ambao wamewahi kutembea juu ya uso wa dunia. Je! Hivi tunaweza kuwazia malaika-mjumbe wa saba aliyechaguliwa na Mungu kutuambia maneno haya:

Ninawapenda. Loo, ninawapenda kana kwamba mlikuwa ni watoto wangu binafsi, nanyi ni watoto wangu katika Injili. Nimewazaa kwa Kristo, kwa njia ya Injili.

Mungu anatujali sana hata Yeye alitutumia nabii Wake aliyethibitishwa akiwa na ishara ya Nguzo ya Moto kutufanya tujue ya kwamba haikuwa tu ni mtu huyu aliyekuwa akitembea pamoja nasi, bali ilikuwa ni Mungu papo hapo juu yake. Yeye ndiye anayeongoza njia.

Kwa sababu anatujali, kabla ya hukumu iliyo kuu haijaja, ameiandaa njia ambayo tutakuwa huru na hukumu zote zinazokuja. Njia hiyo ya kuepukia ni kwa ajili yetu sisi tu, Wateule. Sisi ndio tumeikubali seli zazi hii ya Uhai. Sisi ndio tuliokusudiwa tangu awali kuliona. Sisi ndio tulio na Ufunuo wa huduma hii kuu ya kanda.

Yeye aliifia huduma hii. Alikufa kusudi Roho Mtakatifu aweze kuwa hapa siku hizi kuonyesha mambo haya. Yeye alikujali. Alijali kuuleta hapa. Alijali kutoa tamshi. Alijali kwa kuwa alikupenda. Alijali vya kutosha kufanya jambo hilo, kumtuma Roho Mtakatifu kwenye hili, kuifanya huduma hii leo.

Kama umechaguliwa tangu zamani kwa Uzima wa Milele, utalisikiliza na utalifurahia. Ni Faraja yako. Ndicho kitu ambacho umekitamani maishani mwako mwote. Ni ile Lulu ya thamani kuu. Tunaachana na kila kitu kwa ajili ya Ujumbe huu, Sauti hii. Ni Bwana wetu Yesu Kristo akizungumza nasi.

Hakuna mtu anayepaswa kutubembeleza-bembeleza, SISI NI WAAMINIO, hakuna kitu kinachoweza kuliondoa kwetu. Hatujali yale mtu ye yote asemayo, tunaamini kila Neno.

Yeye anatujali sana; ikiwa tunahitaji uponyaji, tunaamini tu Neno Lake kutoka ndani kabisa ya kilindi cha moyo wetu. Basi haijalishi mshauri yeyote, mfariji ye yote, daktari ye yote, hospitali yo yote, ubaini wowote ungesema nini, tunaamini tu Neno Lake. Tunajua tu hilo! Hakuna haja ya kusema jambo lingine lolote kulihusu; tunajua hilo.

Yeye alitujali sana hata akamfanya nabii Wake akihifadhi Chakula kwa ajili ya Bibi-arusi Wake. Aliagiza hata kila mchungaji, mhudumu, na kundi la watu ulimwenguni kote kufuata maagizo yake na kuzicheza kanda hizi katika MAKUSANYIKO ama makundi yao.

Kama ninyi watu mtafanya hivyo asubuhi ya leo, mtakaoombewa Na ninyi watu mnaoisikia kanda hii, kote ulimwenguni, na baada ya kanda hii kuchezwa na mhudumu ama mtu anayeicheza katika makundi ya kusanyiko huko misituni ama popote mlipo, mnaoicheza, kwanza mtafanya toba yenu dhahiri, kisha mje bila chochote moyoni mwenu, ila imani, na kuombewa, hapo ndipo Dawa itakapofanya kazi.

Nilidhani wakosoaji wetu wanasema kuwa nabii HAKUSEMA kucheza kanda kanisani? Si tu kwamba Yeye alisema katika makanisa yao, bali katika misitu ama POPOTE mlipo…CHEZENI KANDA.

Kama utatii na kufanya yale hasa Mungu aliyonena kupitia malaika-mjumbe Wake wa saba aliyethibitishwa, basi wewe pia unaweza kuwa na IMANI kuu kuliko zote unayoweza kuwa nayo.

Kwanza, na kulikaribia hili, wasikilizaji hawana budi kutiwa mafuta kwa imani. Wewe, kama huna imani, basi hakuna—hakuna hata haja ya kuja kuombewa, kwa maana itahitaji imani yako na imani yangu pamoja; imani yangu kumwamini Yeye,imani yako kumwamini Yeye.

Sisi hatudhanii, ama kukisia, ama kutumainia ni hivyo. Kanda ndiyo Njia ya Mungu iliyoandaliwa ya siku hii. Si maneno ya mtu anayeitwa William Marrion Branham, Ni Maneno yaliyofunuliwa ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kabisa ni, “Amina!” Ndio mkataa wetu. Ni Kweli na si kitu ila Kweli tupu.

Na unapoupata Mkataa wa Mungu, Neno Lake, ahadi juu ya jambo fulani, inakubidi kujua kwanza ya kwamba ni Neno la Mungu, ya kwamba jambo unaloliona likitekelezwa ni Mungu. Ha—hakuna—hakuna “huenda ikawa ndivyo, ingewezekana, inaonekana kana kwamba huenda ikawa.” “Ni Mungu!” Ndipo unapofikia mahali hapo, basi hiyo ndiyo ile Lulu ya thamani kubwa, huna budi kuachana na chochote mtu yeyote anachokwambia kinyume Chake. Haikupasi kuangalia kile mwanadamu ametimiza.

Tunakwenda kuwa na KARAMU KUBWA MNO YA UPENDO Jumapili hii. Tutafanya kile ambacho malalika-mjumbe wa saba wa Mungu aliyethibitishwa aliyotuambia tufanye: Bonyeza Play na kutii.

LOLOTE tunalohitaji, tutalipokea. Tutalipokea kwa sababu tutaiweka imani yetu pamoja na IMANI YAKE kumwamini Yeye. Kisha sote tutasema:

Tangu sasa na kuendelea, kuna kitu moyoni mwangu kinachoniambia ya kwamba shida zangu zimekwisha. Mimi ni—mimi ni mzima, nitapona”? Mnaamini hilo? Inueni mikono yenu, “Ninaamini Hilo!” Mungu awabariki.

Kwa sababu Mungu anajali, ninakualika uje kuungana nasi; ama umtie moyo mchungaji wako, kiongozi wako, kufuata maagizo ya nabii, na kumsikia malaika wa saba wa Mungu akinena Neno la Mungu na upokee lolote unalohitaji, Jumapili hii saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville ( Ni saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki ) tunaposikia: 63-0721 Yeye Hujali. Je! Wewe Unajali?

Ndugu. Joseph Branham

Maandiko ya kusoma kabla ya ibada:

Yohana Mt 5:24 / 15:26
1 Petro 5:1-7
Waebrania 4:1-4

23-1029 Mfungwa

UJUMBE: 63-0717 Mfungwa

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Jumamosi.

Wapendwa Wafungwa,

Maisha yako unayoishi sasa yataakisi maisha ambayo ungeishi ikiwa ungeishi katika siku za Nuhu, ama Musa, kwa sababu una roho yule yule. roho yeye yule aliye ndani yako sasa alikuwa ndani ya watu wakati huo.

Kama ungaliishi katika siku za Nuhu, ungechukua upande wa nani wakati huo? Je, ungeingia kwenye mashua pamoja na Nuhu ukiamini kwamba yeye ndiye ambaye Mungu alimchagua kujenga safina na kuwaongoza watu, au ungesema, “Mimi naweza kujenga safina pia. Mimi ni mzuri tu kama nahodha na mjenga mashua”?

Vipi kama ungaliishi katika siku za Musa? Je, ungekaa na Musa na kuamini kwamba yeye ndiye ambaye Mungu alimchagua kuwaongoza watu, ama ungeenda pamoja na Dathani na Kora waliposema “Sisi pia ni watakatifu, tunalo jambo la kusema. Mungu alituchagua sisi pia.”?

Kila mmoja wetu anapaswa kuchagua, leo hii, kati ya mauti na uzima. Sijali wewe unasema uko upande gani. Yale unayofanya, kila siku, yanathibitisha kile ulicho. Tunabonyeza Play KILA SIKU.

Je, uko katika Neno kila siku? Je, unaomba, ukitafuta Mapenzi makamilifu ya Bwana katika kila jambo unalofanya? Je, unabonyeza play na kuisikia Sauti ya Mungu iliyothibitishwa kila siku? Je, unaamini ni muhimu kabisa Kubonyeza Play? Je! unaamini hiyo Sauti iliyo kwenye kanda ni Sauti ya Mungu kwa ajili ya siku hii?

Kwetu sisi, jibu ni NDIYO. Tunauambia ulimwengu kwamba sisi ni Wafungwa wa Neno la Mungu, Ujumbe Wake, Sauti ya Mungu iliyothibitishwa kwa ajili ya siku yetu. Ndiyo, tunaamini Kubonyeza Play kwa moyo wetu wote. Ndiyo, tunaamini mjumbe wa wakati wa 7 wa kanisa ndiye aliyeitiwa kumwongoza Bibi-arusi. Ndiyo, hiyo Sauti iliyo kwenye kanda ndiyo Sauti muhimu zaidi yakusikia.

Upendo wa Mungu, Sauti Yake, Ujumbe huu, ni mkuu sana, Ufunuo kama huu kwetu sisi, kwamba hatuwezi kamwe kuuacha. Tumekuwa Mfungwa Kwa jambo hilo.

Tumeuza kila kitu kingine. Haidhuru mtu mwingine yeyote anasema nini, tumefungiwa hatamu Kwake. Kuna jambo fulani kulihusu hili ambalo kamwe hatuwezi kuliacha. Ndio furaha ya maisha yetu. Hatuwezi kuishi bila hilo.

Tuna furaha sana, tunashukuru sana, tunajivunia kuwa Mfungwa kwa ajili ya Bwana na Ujumbe Wake; maana ni mamoja. Ni zaidi ya uhai kwetu. Kila siku inakuwa wazi na halisi zaidi kwamba sisi ni Bibi-arusi Wake. Tuko katika Mapenzi yake makamilifu. Tunaweza kunena Neno, kwa maana sisi ni Neno lililofanyika mwili.

Hatujaunganishwa na chochote ila Kristo na Ujumbe Wake wa saa; hata baba zetu, mama zetu, Ndugu zetu, dada zetu, waume zetu, wake zetu, yeyote yule. Tumeunganishwa tu na Kristo, na Yeye pekee. Tumeunganishwa na kufungwa nira kwa Ujumbe huu, Sauti hii, kwa maana ndiyo Njia ya Mungu iliyoandaliwa kwa ajili ya siku hii, WALA HAKUNA NJIA NYINGINE.

Sisi si wafungwa tena wa utu wetu wenye ubinafsi, wa lengo letu. Tumejitolea kabisa na kufungwa nira Kwake. Haidhuru ulimwengu wote unawaza nini, vile hao wengine ulimwenguni wanavyofanya, tumefungwa kwa vifungo vya upendo Kwake na Sauti Yake.

Tunashukuru sana sisi kuwa Wafungwa. Nieleze, Baba, nini cha kufanya kila sekunde ya kila dakika ya kila siku. Hebu na Sauti Yako itufundishe katika kila jambo tunalofanya, tunalosema, na jinsi tunavyotenda. Hatutaki kujua kingine ila Wewe.

Njoo ufungwe hatamu pamoja nasi kwa Neno la Mungu na Sauti Yake Jumapili hii saa 6:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,( Ni saa 1:00 MOJA JIONI ya Afrika Mashariki) tunaposikia jinsi ya kuwa: Mfungwa 63-0717.

Ndugu. Joseph Branham

Maandiko ya kusoma kabla ya Kusikiliza Ujumbe:

Filemoni 1:1

Maelezo ya ziada:
Ndugu Branham, TUNAPENDA jinsi unavyotamka Filemoni, ni KAMILIFU kwa Bibi-arusi.

23-1022 Mbona Unalialia? Nena!

UJUMBE: 63-0714M Mbona Unalialia? Nena!

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Wapendwa maskani za Mungu,

Mimi ni Kanisa Lake. Wewe ni Kanisa Lake. Sisi tu maskani ambamo Mungu anakaa ndani yake. Sisi ni Kanisa la Mungu aliye hai; Mungu aliye hai akiishi katika nafsi zetu. Matendo yetu ni matendo ya Mungu. Utukufu!!

Sote tunakusanyika pamoja, katika maeneo madogo kutoka kote ulimwenguni; sote tukikusanyika pamoja ilipo Sauti ya Mungu, Neno Lake la siku hii.

Ni ajabu sana. Hakuna kufungwa kwa kitu kingine, ila kwa Yesu Kristo na Neno Lake. Hilo Ndilo, mwisho wa maneno. Tumeketi pamoja katika ulimwengu wa Roho tukikamilishwa na Sauti ya Mungu mwenyewe.

Tunaenda kabisa. tunaenda sote kwenye Nchi ya Ahadi. Kila mmoja wetu! Hata kama wewe ni mke wa nyumbani, u yaya mdogo, mama kizee, babu ama kijana mwanamume, chochote ulicho, tutaenda sisi sote. Hakutakuwa hata na mmoja wetu atakayeachwa nyuma. Kila mmoja wetu ataenda, na “hatutazuiwa na kingine chochote.”

Tunaamini kwamba tunapaswa kuwa wote pamoja. Kundi moja kubwa lililoungana la Mwili wa Yesu Kristo, linalongojea kule Kuja kwenye utukufu. Hatungepaswa kutengana, lakini mwanadamu ametoka kwenye njia iliyowekwa ya mafundisho ya Injili.

Yabidi kuwe njia fulani ya kuonyesha kabisa ni ipi iliyo kweli na iliyo makosa. Na njia pekee utakayotenda, ni kutokuweka fasiri yo yote kwenye Neno, lisome tu jinsi lilivyo na uliamini hivyo. Kila mtu anaweka fasiri yake mwenyewe, na inalifanya linene jambo lingine tofauti. Kuna SAUTI YA MUNGU MOJA tu KWA BIBI-ARUSI. BONYEZA PLAY!

Nayasema kwa kanda hii na kwa wasikizaji hawa; nasema hili chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, “Ni nani aliye upande wa Bwana? Na aje chini ya Neno hili.”

Neno la siku yetu lina Sauti. Nabii wetu ndiye Sauti hiyo. Sauti hiyo ndilo Neno lililo hai kwa ajili ya siku yetu. Tulichaguliwa tangu zamani kuisikia Sauti hiyo na kuona saa hii, na hakuna kitu kitakachotuzuia kuisikia Sauti hiyo.

Imani yetu inaiona hiyo na kuchagua kuisikia hiyo bila kujali mtu yeyote anasema nini. Sisi hatushushi darubini yetu kutazama upande mwingine. Tunaweka kipini chetu cha kulengea shabaha katikati ya Neno kabisa na masikio yetu yametuniwa kwenye Sauti hiyo.

Kwa kujiweka wakfu Kwako Bwana, kutoka mioyoni mwetu hadi Masikioni Mwako, haya ni maombi yetu ya dhati.

Kusudi maisha yetu yapate kubadilika tangu leo na kuendelea, tupate kuwa na mawazo mema. Tutajaribu kuishi vizuri sana na kuwa wanyenyekevu pia tukiamini yale tunayomwomba Mungu, Mungu atampa kila mmoja. Nasi hatutanena maovu sisi kwa sisi ama dhidi ya mtu ye yote. Tutawaombea adui zetu na kuwapenda; tuwafanyie mema wanaotufanyia mabaya. Mungu ndiye Hakimu wa asiye na makosa na aliye na makosa.

Ninawaalika mje kutia mafuta Imani yenu kwa kuisikia Sauti ya Mungu pamoja nasi Jumapili, saa 6:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,( ni saa 1:00 MOJA JIONI ya Afrika Mashariki ) tunaposikia: Mbona Unalialia? Nena! 63-0714M.

Ndugu. Joseph Branham

23-1015 Lile Shtaka Na Ushirika wa Nyumbani Na Kutawadhana Miguu

UJUMBE: 63-0707M Lile Shtaka

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Bibi-arusi wa Kanisa la Nyumbani,

hebu sote tukusanyike pamoja na kusikiliza Ujumbe, Lile Shtaka 63-0707m, Jumapili hii saa 11:00 KUMI NA MOJA JIONI, saa za Jeffersonville. ( Ni saa 6:00 SITA USIKU ya Afrika Mashariki )

Hebu basi na tujitayarishe kwa nafasi iliyo takatifu ya kushiriki Meza ya Bwana majumbani mwetu mara tu baada ya huo Ujumbe huku tukisikiliza 63-0707e Ushirika. Kisha tutakuwa na Ibada ya Ushirika na kutawadhana miguu itafuata. Kama vile Lile shtaka, kanda ya Ushirika itachezwa kwenye Voice Radio (kwa Kiingereza peke yake), ikifuatiwa na muziki wa piano, nukuu ya kutambulisha kutawadhana miguu, na Nyimbo za Injili, kama kawaida tufanyavyo katika ibada za Ushirika za Nyumbani.

Zilizoorodheshwa hapa chini ni anuani za njia za kupata ama kuandaa divai na mkate wa Ushirika.

Ninashukuru sana kwamba Bwana ametuandalia njia ya kumwalika Mfalme wa wafalme katika kila moja ya nyumba zetu kwa siku iliyo maalum sana pamoja Naye. Hakika ninatazamia kukutana nanyi nyote Mezani Pake.

Mungu awabariki,

Ndugu Joseph Branham

Instructions for Baking Bread / Making Wine

Instructions to obtain Communion Wine / Feet Washing Bins

Kampeni za uinjilishaji za kasisi William Branham

Sanduku la Posta 325
Jeffersonville, Indiana

Julai 13, 1964

Ndugu mpendwa Gagnon;
Salamu katika Jina la Bwana.

Ilikuwa ni furaha kusikia kutoka kwako leo hii, na ninaamini kwamba u mzima, ukimtumikia Bwana.

Ilikuwa furaha kuisoma barua yako, na kuona unyoofu wako kwa kuniuliza maswali yafuatayo. Kwa msaada wa Bwana, nitajaribu kukujibu hilo. Kwanza, kuhusu ushirika, Ndiyo, Shiriki, huhitaji kuwa mhudumu ili kufanya jambo hilo; Divai iko sawa. Kuhusu swali kuhusu nambari 666, ni kuhusu tu njia yako ya kuzaliwa tu, na haimaanishi chochote kile, kwa sababu sasa wewe ni mtoto wa Bwana aliyezaliwa mara ya pili.

Natumai nitasikia kutoka kwako tena hivi karibuni.

Katika huduma yake,

Ndugu Branham

BB/wpb

KUMBUKA: Swali nililomuuliza Ndugu Branham ni hili:

Nilimwambia sisi hatuna mhudumu, nasi tulitaka kujua ikiwa ilikuwa ni sawa kwangu kuhudumia ushirika. Pia, ikiwa ilikuwa ni sawa kutumia divai ya “kosher”.

AA Gagnon

23-1008 Je, Maisha Yako Yanaistahili Injili?

UJUME: Je, Maisha Yako Yanaistahili Injili? 63-0630E

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Wapendwa kundi la Nabii wa Mungu,

Tuombe.

Baba wa Mbinguni, jinsi tunavyoshukuru kwa ajili ya wakati mwingine wa kukusanyika pamoja kutoka kote ulimwenguni upande huu wa Umilele. Kuwa katika nia moja na umoja pamoja Nawe; tukiiskia Sauti yako ikituzungumzia. Tunatarajia kwa mara nyingine tena kuhuishwa upya kwa nguvu kuja kutoka Kwako, zipate kututia moyo na nguvu kwa ajili ya safari iliyoko mbele.

Tunakusanyika pamoja ili kuipokea Mana iliyotolewa kwa ajili yetu. Ile Mana ya kiroho uliyoihifadhi ili itupe nguvu kwa ajili ya safari. Ndilo jambo PEKEE linaloweza kutuhifadhi katika siku zijazo.

Ulituambia, kabla hujaliweka Kanisa Lako katika utaratibu, itabidi utukusanye pamoja, mahali pamoja, na kwa nia moja. Ndipo ungemtuma Roho wako Mtakatifu kwetu kwa ajili ya uongozi; si baraza fulani la ekumeni, si kundi fulani la watu, bali Roho Wako Mtakatifu atuzungumzie mdomo kwa sikio.

Wewe ulinena kupitia malaika wako na kutuambia:

“Ninawatakeni mkae na mchungaji wenu na mdumu na Mafundisho ambayo yamefundishwa hapa. Dumuni na Neno hili, msiliache! Dumuni moja kwa moja na Neno hata iweje, dumuni na Neno hilo!”

Baba, tunalitii Neno Lako nasi tunakaa na mchungaji wetu. Ni Sauti ya Mungu kwa ajili ya siku hii tu ndiye anenaye Neno Lako lililo safi ambalo limethibitishwa na kudhihirishwa kwa ajili ya siku yetu.

Ulituambia kama ilivyokuwa katika siku za Sodoma, ndivyo itakavyokuwa katika Kuja kwake Mwana wa Adamu; kwamba tungekuwa na mambo mawili ya kutuongoza, na ulimwengu wote uliyosalia ungekuwa na mambo mawili. Mambo yao mawili walikuwa wahubiri wawili.

Lakini kwa ajili ya Kanisa Lako la kiroho, Bibi-arusi Wako mteule, aliyechaguliwa tangu zamani, mambo yetu mawili yangekuwa ni Wewe, kudhihirishwa katika mwili wa kibinadamu, kutuongoza kwa Nguzo ya Moto.

Acha upepo uvume vikali. Acha tufani itikise. Tuko salama, milele. Tunapumzika papo hapo kwenye Neno Lako. Wakati umefika. Kule kutoka kwa kiroho kumewasili. Tunatembea na kuzungumza nawe kila siku, tukisikia Sauti Yako. Tuko katika ushirika wa daima na Wewe.

Tunataka kuwa Mikono Yako, Macho Yako, Ulimi Wako. Wewe ni mzabibu, sisi ni matawi Yako. Tutie nguvu, Baba, ili tuzae matunda yako. Nia yetu pekee ni kuwa na maisha yanayoistahili Injili Yako.

Jihakisi Mwenyewe kupitia sisi, Baba, ili kuendeleza kazi Yako na kutimiza Neno Lako lililoahidiwa. Nia yetu ni kuwa wajumbe Wako wa siku hii, ili kuitimiza haki yote.

Tunataka kukusikia Wewe ukituambia:

Ombi langu ni kwamba, kwa wale walioko kwenye redio ama kwenye…kwenye maeneo ya kanda, na wale waliopo hapa. Mungu wa neema yote, wa Mbinguni, na atuangazie sisi sote Roho Wake Mtakatifu, kusudi sisi, tangu usiku huu, kuendelea, tunaweza kuishi maisha ambayo Mungu angesema, “Nimependezwa. Ingieni katika furaha za Milele ambazo zimewekwa tayari kwa ajili yenu tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.” Mungu wa Mbinguni na atume baraka Zake juu yenu nyote.

UTUKUFU…hao ni sisi Baba, Bibi-arusi Wako katika maeneo ya kanda. Hakika Wewe unatutumia baraka zako na kutufunulia Neno lako, ukituambia kwa kila Ujumbe tunaousikia, Wewe umependezwa, SISI NI BIBI-ARUSI WAKO.

Ikiwa ungependa kumsikia mchungaji wetu, mchungaji wa Mungu kwa ulimwengu mzima ambaye Yeye alimtuma kumwita atoke na kumwongoza Bibi-arusi Wake, njoo uungane nasi Jumapili saa 6:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville, ( ni saa 1:00 MOJA JIONI ya Afrika Mashariki ) kumsikia Yeye akinena Maneno ya Uzima wa Milele, anapotuletea Ujumbe kutoka kwa Mungu: Je, Maisha Yako Yanaistahili Injili? 63-0630E.

Ndugu. Joseph Branham

Tangazo Maalum: Bwana akipenda, Jumapili ijayo usiku, tarehe 15 Oktoba. tutakuwa na Ibada ya Ushirika ya nyumbani na Kutawadhana Miguu.

23-1001 Kutoka Kwa Tatu

UJUME: 63-0630M Kutoka Kwa Tatu

PDF

pakua – m4a

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Bibi-arusi wa Kutoka,

Mambo haya tunayoyaona yakitukia leo yasingeweza kutokea miaka ishirini iliyopita, ama miaka arobaini iliyopita; ni leo tu ndio yanafanyika. Hii ndio ile saa! Huu ndio wakati! Sasa ndio wakati wake wa kutimizwa. Mungu aliliahidi, NA NDILO HILI HAPA.

Sisi tuna ufahamu wa kiroho; uovu wa taifa hili umetimia. Ile saa imefika. Ni wakati wa kwenda kwenye ile Nchi ya ahadi. Sio nchi nyingine tu ya kuendea, bali Makao yetu ya Baadaye ambayo tumekuwa tukiyangojea.

Hebu Wazia jambo hilo, kile kinachotuongoza ni zaidi ya nabii. Ni Mungu aliyedhihirishwa katika mwili miongoni mwetu, pamoja na Neno Lake kuthibitisha jambo hilo. Nabii ambaye aliyefanya mara elfu zaidi ya nabii mwingine ye yote. Ni Nguzo ya Moto inayotuongoza kwenda kwenye ile Nchi ya ahadi, Utawala wa Miaka Elfu.

Yeye alimchagua nabii wetu na akampa ishara ya kimbinguni ya Nguzo ya Moto, ili asikosee. Yale nabii aliyosema ni Maneno hasa ya Mungu Mwenyewe. Alimchukua nabii wetu, akamfundisha, kisha akamrudisha kwetu pamoja na ile Nguzo ya Moto, ili ajithibitishe Mwenyewe kwetu, na kutupa Ufunuo mkamilifu wa Neno Lake lote.

Kama tunataka kwenda kwenye hiyo Nchi ya ahadi, hatupaswi kusahau kamwe, Mungu hawezi, na hatabadilisha mpango Wake. Yeye ni Mungu, Naye hawezi. Alituambia Yeye kamwe hatajishughulisha na Kundi. Hajawahi kamwe. Yeye hutushughulikia kama mtu mmoja-mmoja. Yeye alituahidi katika Neno Lake angetutumia Malaki 4 atuongoze kwenda kwenye Nchi hii, Naye ametutumia.

Lakini, unaona, Ahabu alikuwa na mfumo aliodhani ulikuwa ni wa Bwana. Akasema, “Nina mia nne wa hao, walioelimishwa na kufundishwa.” Nao wanadai kwamba ni manabii wa Kiebrania, kama vile makundi ya wahudumu yanavyodhani siku hizi.

Wengi hawataki kulikubali, lakini kama Eliya wa kale, Mjumbe-malaika wa saba wa Mungu, mchungaji wetu, ndiye mchungaji wa ulimwengu wote kumwongoza Bibi-arusi Wake.

Yeye ni Malaki 4:5, na Ufunuo 10:7. Yeye ndiye kutimizwa kwa Maandiko yote ambayo Biblia ilitabiri kumhusu. Ni Ujumbe huu, Sauti hii, ambayo ni Sauti ya Mungu inayomwita Bibi-arusi Wake. Ndiyo Ramani ya Mungu kwa ajili ya siku hii.

Ni Nguzo ile ile ya Moto, kwa mfumo ule ule uliotiwa mafuta. Mungu yeye yule akifanya mambo yale yale.

Sasa Neno limefanyika mwili na linaishi kati yetu katika miili yetu, Bibi-arusi Neno Wake.

Hebu na tumlilie na kumshukuru, tumsifu, tumwabudu, kwa yote aliyotenda: Kutuokoa, kutuchagua tangu zamani, kutuhesabia haki.

Yale Anayotufanyia sasa hivi; Yanatupa Ufunuo na Ufunuo, akituambia sisi ni nani. Na yote atakayotufanyia…Kuja kutuchukua kuwa Bibi-arusi Wake na kutupeleka kwenye Makao yetu ya Baadaye Aliyotuandalia, na kuwa pamoja Naye katika Milele yote.

Chochote tunachohitaji, mlilie Yeye. Hilo ndilo analotaka watoto Wake wafanye. Kumlilia Yeye mpaka tumeridhika na kupata kile tunachokihitaji.

Njoo ukaungane na sehemu ya Bibi-arusi Wake Jumapili saa 6:00 SITA MCHANA, saa Jeffersonville, ( Ni saa 1:00 MOJA JIONI ya Afrika Mashariki ) na umsikie mchungaji wa Mungu kwa ulimwengu, William Marrion Branham, akituambia yote kuhusu: Kutoka kwa Tatu 63-0630M.

Ndugu. Joseph Branham

Maandiko ya kusoma kabla ya Ujumbe:

Kutoka 3:1-12
Mwanzo Sura ya 37 yote
Mwanzo Sura ya 43 yote

23-0924 Kimulimuli Chekundu Cha Dalili Ya Kuja Kwake

UJUME: 63-0623E Kimulimuli Chekundu Cha Dalili Ya Kuja Kwake

PDF

pakua – mp3 (VGR dynamic audio)

pakua – amr

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Bibi-arusi Asiye na Hofu,

ONYO!! ONYO!! Taa nyekundu inamemetesha. Kule kushushwa kwa pazia kumefika. Yatubidi tuweke kila kitu kando, KILA KITU, na tuwe tayari. Tumefika mwisho. Ule wakati ambao tulikuwa tukiungojea tangu mwanzo umefika. Unabii sasa unatimizwa.

Mungu alimwinua mjumbe-tai Wake mwenye nguvu juu sana katika mbingu kutazama miaka sitini ng’ambo ya mwaka 1963 hadi leo, Septemba mwaka 2023, kuyaona yote ambayo yangetendeka katika siku yetu… hali ambayo ulimwengu ungekuwemo, ukosefu wa uadilifu wa wanawake, kanisa na hali yake, wazimu wa watu; mwovu, kipofu, uchi, kahaba mkuu katika matawi yote ya serikali, ufisadi katika siasa, naye ametuonya ni yapi yangetukia.

Sasa tunaliona hilo likidhihirishwa mbele ya macho yetu vile hasa alivyotuambia ingekuwa. Sisi ndio wale walioyaona mambo haya yote yakitimia. Kila kitu kiko mahali pake. Limekuwa chungu kubwa mno la uchafu.

Ulimwengu wote uko katika hali ya hofu. Wanajua hakuna tumaini lililobakia. Inazidi kuwa mbaya kila siku. Hofu imetanda uso wa Dunia. Uchumi umekwisha, mauaji ya bila sababu, wanawake wanataka kuwa wanaume, wanaume wanataka kuwa mwanamke. Cho chote na kila kitu kinakubaliwa. kitu gani kinaweza kutokea wakati wo wote? Wanajua ni kama volkeno; Kitalipuka sekunde yo yote. Unaliona jambo hilo kwenye nyuso zao, katika matendo yao, HAKUNA TUMAINI, HOFU.

Hata makanisa yanayojiita ya Kikristo yanakumbatia watu waliobadili jinsia kuwa wachungaji, viongozi wa kiroho wa watu. Imekuwa mbaya zaidi kuliko Sodoma na Gomora. Shetani na ufalme wake wanaungana na kuwa kitu kimoja. Yeye amelifikia lengo lake.

LAKINI UTUKUFU KWA MUNGU, katikati ya mchafuko huo wote na hofu, Baba ametuhifadhi, SISI, kundi lake la watu teule, Bibi-arusi kipenzi Wake, salama Mikononi Mwake nasi tuna muungano wa Kiroho pamoja Naye zaidi ya wakati wo wote ule. Huu ni wakati mkuu zaidi wa maisha yetu. Ni ajabu. Ni tukufu. Ni la kimbinguni. Ni zaidi ya maneno ambayo tungeweza kueleza.

Miili yetu inafanyika Neno, nalo Neno linafanyika mwili; linadhihirishwa, linathibitishwa. Vile vile hasa Biblia ilivyosema ingetendeka katika siku hii, inatendeka, siku baada ya siku.

Mambo yanatukia na kutendeka upesi sana hivi kwamba hatuwezi hata kufuatilia jambo hilo. Tuko karibu sana na kule Kuja kwa Bwana wetu Yesu; kuunganishwa Naye, ambapo Neno linafanyika Neno.

Pamoja na mambo haya yote yanayotukia kutuzunguka pande zote, HATUJAWAHI KAMWE KUWA NA FURAHA, kuridhika zaidi ama kutosheka zaidi hivi. Mioyo na nafsi zetu zinabubujika kwa furaha isiyotamkika na iliyojaa utukufu. Ni kitendawili.

Tunapata faraja kuliko wakati mwingine wo wote ule, tukijua kwamba tangu mwanzo kabisa, tulichaguliwa tangu zamani kuwa mwana na binti wa Mungu.

SISI ni Bibi-arusi mwadilifu wa Kristo, aliyeoshwa kwa Damu ya Kristo. Mwana wa Mungu wa thamani, mwadilifu, asiye na dhambi akiwa amesimama na Bibi-arusi Neno asiye na doa, asiyeghoshiwa, aliyemwosha kwa Maji ya Damu Yake Mwenyewe. Sisi tulichaguliwa tangu zamani katika kifua cha Baba kabla ya mwanzo wa wakati; kama vile alivyokuwa Yeye ….UTUKUFU!! HALELUYA!

Sisi si hivyo tu tulivyo, lakini hivi karibuni tunaenda kwenye arusi huko mbinguni, tukiwa tumevaa utepe wa arusi ya waliochaguliwa tangu zamani. Alitujua SISI…Hebu tafakari tu juu ya hilo, ALITUJUA kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, kwa hiyo akatuvisha utepe wa arusi PALE na akaliandika JINA LETU KWENYE KITABU CHAKE CHA UZIMA CHA MWANA-KONDOO, si tu kusamehewa, bali KUHESABIWA HAKI.

Kuna njia moja tu ya kuwa na haya yote, yakubidi uje kwa Njia pekee iliyoandaliwa na Mungu. Neno la asili, BONYEZA PLAY.

Tunashukuru sana tunao Ufunuo huu. Ni wazi sana kwetu. Mwili na damu havikutufunulia jambo Hilo, lakini Baba yetu wa Mbinguni na hakuna maneno katika msamiati wetu wa kumwelezea jinsi tunavyompenda Yeye kwa ajili ya Jambo hilo….NEEMA YA AJABU.

Hakuna cha kulinganishwa na kuisikia Sauti ya Mungu ikikuzungumzia mdomo kwa sikio. Furaha inayofurika mioyo yetu. Hakuna kushangaa, hakuna kubahatisha, hakuna, hata si kutumaini, TUNAJUA, NI BWANA ASEMA HIVI. Huwezi kuwa na uhakika huo wa 100% mahali pengine popote isipokuwa kwenye kanda.

Ningependa kukualika uje uungane pamoja nasi tunapoisikia Sauti ya Mungu ikituambia yote kuhusu siku tunayoishi, wakati yeye anaponena kupitia nabii-tai Wake mwenye nguvu na kutuletea Ujumbe: Kimulimuli Chekundu cha Dalili ya Kuja Kwake 63-0623E.

Tutakusanyika kutoka kote ulimwenguni saa 6:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville ( ni saa 1:00 MOJA JIONI ya Afrika Mashariki). Kama huwezi kuungana nasi pamoja, popote pale ulipo, lo lote lile ufanyalo, Bonyeza Play na uyasikie Maneno ya Uzima wa Milele.

Ndugu. Joseph Branham

Maandiko ya kusoma kabla ya kusikiliza Ujumbe:

Mathayo 5:28 / 22:20 / Sura ya 24 yote
2 Timotheo Sura ya 4 yote
Yuda 1:7
Mwanzo Sura ya 6 yote