Pasaka 2024

Mpendwa Bibi-arusi wa Kristo,

Kalvari inapaswa kukumbukwa kila siku. Tumesikia mengi sana kuihusu. Tumesoma mengi sana juu yake. Wahubiri wameihubiri tangu mwanzo wa wakati. Waimbaji wameimba juu yake katika nyakati zote. Manabii walitabiri miaka elfu nne kabla haijatukia, na manabii wa siku hizi wanatuonyesha kule nyuma ilipotendeka. Ni siku muhimu sana.

Ni moja ya siku zilizo muhimu sana ambazo Mungu amepata kuzishusha duniani.

Ni kukusanyika kwa kipekee kulikoje kutoka ulimwenguni kote ambako Bibi-arusi atakuwanako wikendi hii ya Pasaka. Tutafunga milango yetu na kuuzima ulimwengu wa nje. Tutazima vifaa vyetu vyote ili tusizubaishwe, na tuongee Naye kabisa kabisa kila siku. Tutainua sauti zetu kwake kwa upatano, kwa nia moja na moyo mmoja, kumsifu, kumwabudu, kumwambia jinsi gani tunavyompenda.

Tutasikia Sauti Yake ikizungumza na mioyo yetu tunapoyaweka upya maisha yetu Kwake. Hakuna kitakachokuwa muhimu zaidi kwetu wakati tunapojitayarisha kwa ajili ya Ujio Wake wa hivi karibuni. Bibi-arusi anajiweka mwenyewe tayari zaidi ya hapo awali.

Ningependa sote tuungane kwenye ratiba ifuatayo:

ALHAMISI

Ilikuwa ni Alhamisi usiku ambapo Bwana Yesu alikula Karamu ya Mwisho na wanafunzi wake, katika ukumbusho wa Pasaka kabla ya kule kutoka kwa wana wa Israeli. Ni fursa iliyoje tuliyo nayo ya kuzungumza na Bwana katika nyumba zetu, kabla ya wikendi yetu takatifu, na kumwomba atusamehe dhambi zetu, na kutupa sisi sote yale tunayohitaji katika safari yetu.

Lijalie, Bwana. Waponye walio wagonjwa. Wafariji walio wachovu. Wape furaha wanaodhulumiwa. Wape amani walio wachovu, Chakula kwa wenye njaa, Maji kwa wenye kiu, furaha kwa wenye huzuni, uwezo kwa kanisa. Bwana, mlete Yesu miongoni mwetu usiku wa leo, tukiwa tunajitayarisha kushiriki ushirika unaowakilisha mwili Wake uliovunjwa-vunjwa. Tunaomba, Bwana, kwamba Yeye atatuzuru kwa njia ya ajabu sana…

Wabariki wengine, Bwana, kila mahali ulimwenguni, ambao wanangojea kwa furaha kuja kwa Bwana, taa zimetengenezwa, na dohani zimesuguliwa kabisa, na Nuru ya Injili ikiangaza katika sehemu zenye giza.

Hebu sote tuanze saa 12:00 KUMI NA MBILI JIONI. Masaa ya maeneo mnayoishi ili kusikia  Ushirika 62-0204, na kisha nabii atatupeleka katika Ibada yetu maalum ya Ushirika na Kutawadhana Miguu, ambayo itakuwa ikicheza kwenye app ya Lifeline (kwa Kiingereza), au unaweza kupakua ibada hii kwa Kiingereza ama lugha nyinginezo kwa kubofya anuani iliyo hapa chini.

Kufuatana na Ujumbe, tutakusanyika pamoja na familia zetu katika nyumba zetu na kula Meza ya Bwana.

IJUMAA

Hebu tuende katika maombi pamoja na familia zetu saa 3:00 TATU ASUBUHI,( ni saa 10:00 Kumi jioni ya Afrika Mashariki ) na kisha tena saa 6:00 SITA MCHANA,( ni saa 1:00 Moja jioni ya Afrika Mashariki ) tukimualika Bwana awe pamoja nasi na azijaze nyumba zetu na Roho Mtakatifu wakati tujiweka wakfu Kwake.

Hebu mawazo yetu na yarudi nyuma hadi siku ile pale Kalvari, zaidi ya miaka 2000 iliyopita, na kumwona Mwokozi wetu akining’inia msalabani, na kisha tujitoe vivyo hivyo kufanya daima yale yanayompendeza Baba:

Iwapo siku hii ni muhimu sana, moja ya siku zilizo kuu sana, hebu na tuangalie mambo matatu ambayo siku hiyo ilimaanisha kwetu. Tungechukua mamia. Bali asubuhi ya leo nimechagua tu mambo matatu tofauti yaliyo muhimu sana ambayo tunataka kuyachunguza katika muda mfupi ujao; ambayo Kalvari ilimaanisha kwetu. Nami naomba ya kwamba itamhukumu kila mwenye dhambi aliyeko, ya kwamba itamfanya kila mtakatifu kupiga magoti yake, ya kwamba itamfanya kila mgonjwa ainue imani yake kwa Mungu na aondoke ameponywa, kila mwenye dhambi aokolewe, kila aliyerudi nyuma arudi na ajionee aibu, na kila mtakatifu afurahi na apate tumaini jipya na tumaini jipya.

Kisha saa 6:30 SITA NA NUSU MCHANA,( Ni saa 1:30 Moja na Nusu jioni ya Afrika Mashariki ) tuungane pamoja katika nyumba zetu ili kusikia,  Siku Hiyo Pale Kalvari 60-0925.

Kisha tuungane tena pamoja katika maombi saa 9:00 TISA ALASIRI.( ni saa 4:00 Nne Usiku ya Afrika Mashariki ) katika ukumbusho wa kusulubishwa kwa Bwana wetu.

JUMAMOSI

Hebu sote kwa mara nyingine tena tuungane katika maombi saa 3:00 TATU ASUBUHI.( ni saa 10:00 Kumi jioni ya Afrika Mashariki ) na  saa 6:00 SITA MCHANA,( ni saa 1:00 Moja Jioni ya Afrika Mashariki ) na kuitayarisha mioyo yetu kwa ajili ya mambo makuu Atakayotutendea sisi katikati yetu.

Ninaweza kumsikia akisema, “Shetani, njoo hapa!” Yeye ni Bosi sasa. Ananyosha mkono, anaunyakua ule ufunguo wa mauti na kuzimu kutoka ubavuni mwake, akauning’iniza ubavuni Mwake Mwenyewe. “Ninataka kukupa notisi. Umekuwa laghai muda mrefu kutosha. Mimi ni Mwana wa Mungu aliye hai niliyezaliwa na bikira. Damu Yangu ingali imelowa msalabani, na deni kamili limelipwa! Huna haki tena. Umenyang’anywa zote. Nipe funguo hizo!”

Kisha saa 6:30 SITA NA NUSU MCHANA, ( ni 1:30 moja na Nusu jioni ya Afrika Mashariki ) sote tutakusanyika ili kusikia NENO:  Kuzikwa 57-0420.

Hii itakuwa SIKU-KUU iliyoje kwa Bibi-arusi Wake ulimwenguni kote.

Kisha tuungane tena pamoja katika maombi saa 9:00 TISA ALASIRI ( Ni saa 4:00 Nne Usiku ya Afrika Mashariki ).

JUMAPILI

Hebu kwanza tuamke mapema kama Ndugu Branham alivyofanya asubuhi ile wakati rafiki yake mdogo, robin, alipomwamsha saa 11:00 KUMI NA MOJA ASUBUHI. Hebu tumshukuru tu Bwana kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu:

Saa kumi na moja asubuhi ya leo, rafiki yangu mdogo mwenye kifua chekundu aliruka dirishani akaniamsha. Ilionekana kana kwamba moyo wake mdogo ungepasuka, akisema, “Amefufuka.”

Saa 3:00 TATU ASUBUHI. ( Ni saa 10:00 Kumi jioni ya Afrika Mashariki ) na saa 6:00 SITA MCHANA,( ni saa 1:00 Moja jioni ya Afrika Mashariki ) hebu tuungane kwa mara nyingine tena katika mnyororo wetu wa maombi, kuombeana mmoja kwa mwingine na kujitayarisha wenyewe kuisikia Sauti ya Mungu.

Saa 6:30 SITA NA NUSU MCHANA, ( Ni saa 1:30 Moja na Nusu jioni ya Afrika Mashariki ) tutakusanyika pamoja ili kuusikia Ujumbe wetu wa Pasaka:  Muhuri wa Kweli wa Pasaka 61-0402.

Saa 9:00 TISA ALASIRI, ( ni saa 4:00 Nne usiku ya Afrika Mashariki ) tuungane tena katika maombi, tukimshukuru Yeye kwa WIKENDI YA AJABU ALIYOTUPA PAMOJA NAYE NA PAMOJA NA BIBI-ARUSI WAKE ULIMWENGUNI KOTE.

Kwa ndugu na dada zangu walio nchi za ng’ambo, kama mwaka jana, ningependa kuwaalika kuungana nasi kwa masaa ya Jeffersonville, kwa masaa yote ya maombi yaliyo kwenye ratiba hii. Ninatambua, hata hivyo, kwamba kuzicheza Kanda ya Alhamisi, Ijumaa, na Jumamosi alasiri kwa masaa ya Jeffersonville kungekuwa vigumu sana kwa wengi wenu, kwa hivyo tafadhali jisikieni huru kucheza Jumbe hizo kwa masaa yafaayo kwenu. Ningependa, hata hivyo, tuungane pamoja Jumapili saa 6:30 SITA NA NUSU MCHANA, saa za Jeffersonville, ( ni saa 1:30 MOJA NA NUSU Jioni masaa ya Afrika Mashariki ) ili kuusikia Ujumbe wetu wa Jumapili pamoja.

Ningependa pia kuwaalika ninyi na watoto wenu kuwa sehemu ya vipindi vya Ubunifu, Journaling, na maswali ya majaribio ya YF, ambayo familia yako yote yaweza kufurahia pamoja. Twaamini utayapenda kwa kuwa yote yanahusiana na NENO tutakalosikia wikendi hii.

Kwa ratiba ya wikendi, taarifa ya jinsi ya kujiandaa kwa ajili ya ibada ya Ushirika, nyenzo zitakazohitajika kwa ajili ya vipindi vya ubunifu, Maswali ya jaribio la Pasaka, na taarifa nyinginezo, tazama anuani zilizo hapa chini.

Hebu na tuzifunge simu zetu kwa ajili ya wikendi ya Pasaka isipokuwa kupiga picha, kusikia Nukuu ya Siku, na kucheza kanda kwenye app ya the Table, app ya Lifeline, au anuani za kupakua.

Ni heshima kubwa kwangu kukualika wewe na familia yako kukusanyika pamoja na Bibi-arusi ulimwenguni kote katika wikendi iliyojaa KUABUDU, SIFA NA UPONYAJI. Ninaamini kweli hakika ni wikendi ambayo itayabadilisha maisha yako milele.

Ndugu Joseph Branham