Ee Mwana-Kondoo wa Mungu, Wewe ndiwe Zawadi iliyo kuu ya Mungu iliyofungwa kwa ulimwengu. Umetupa Zawadi iliyo kuu kuliko zote iliyowahi kutolewa, Wewe Mwenyewe. Kabla haujaumba nyota ya kwanza, kabla haujaumba dunia, mwezi, mfumo wa jua, ulitujua sisi na kutuchagua tuwe Bibi-arusi Wako.
Ulipotuona wakati huo, ulitupenda. Tulikuwa nyama ya nyama Yako, mfupa wa mfupa Wako; tulikuwa sehemu Yako. Jinsi Ulivyotupenda na kutaka kushirikiana nasi. Ulitaka kuushiriki Uzima Wako wa Milele nasi. Tulijua basi, tungekuwa Bibi JEZU Wako.
Uliona tungeshindwa, kwa hivyo Wewe ulilazimika kuiandaa njia ya kuturudisha sisi. Tulikuwa tumepotea na bila tumaini. Kulikuwa na njia moja tu, Ilibidi Wewe ufanyike “Uumbaji Mpya”. Ilibidi Mungu na mwanadamu wawe Mmoja. Ilibidi Wewe ufanyike sisi, ili sisi tuweze kuwa Wewe. Hivyo, Ukauweka mpango Wako mkuu utende kazi maelfu ya miaka iliyopita katika bustani ya Edeni.
Umetamani sana kuwa pamoja nasi, Bibi-arusi Wako wa Neno kamilifu, lakini Wewe ulijua kwanza Ilikubali uturudishe sisi kwenye yale yote yaliyokuwa yamepotea hapo mwanzo. Ulingoja na kungoja na kungoja hadi siku hii kuukamilisha mpango Wako.
Siku hiyo imefika. Lile kundi dogo uliloliona hapo mwanzo liko hapa. Kipenzi chako anayekupenda Wewe na Neno Lako kuliko kitu chochote.
Ilikuwa ni wakati Wako wa kuja na kujidhihirisha Mwenyewe katika mwili wa mwanadamu kama ulivyofanya kwa Ibrahimu, na kama ulivyofanya ulipofanyika Uumbaji mpya. Jinsi Wewe umeisubiri kwa hamu siku hii ili uweze kutufunulia sisi siri Zako zote kuu zilizofichwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.
Unamjivunia sana Bibi-arusi Wako. Jinsi Wewe unavyopenda kumwonyesha Yeye na kumwambia Shetani, “Hata ujaribu kuwafanyia nini, wao hawataondoshwa; hawatapatana kuhusu Neno Langu, Sauti Yangu. Wao ni BIBI-ARUSI Wangu wa NENO KAMILIFU.” Wao ni wakupendeza sana Kwangu. Hebu Watazame tu! Kupitia majaribio na majaribu yao yote, wao wanabaki waaminifu kwa Neno Langu. nitawapa zawadi ya milele. Yote niliyo Mimi, Nawapa wao. TUTAKUWA MMOJA.
Tunachoweza tu kusema ni: “JEZU, TUNAKUPENDA. Jalia tukukaribishe nyumbani mwetu. Hebu na tukupake Wewe mafuta na tuioshe miguu Yako kwa machozi yetu na kuibusu. Hebu na tukuambie jinsi tunavyokupenda Wewe.”
Yote tuliyo, tunakupa wewe JEZU. Hiyo ndiyo zawadi yetu Kwako JEZU. Tunakupenda. Tunakuhimidi. Tunakuabudu.
Ninawaalika kila mmoja wenu aungane nasi Jumapili saa 6:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,(Ni saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki) na umkaribishe JEZU nyumbani kwako, kanisani kwako, ndani ya gari lako, popote uwezapo kuwa, na uipokee Zawadi iliyo kuu kuliko zote iliyowahi kutolewa kwa mwanadamu; Mungu Mwenyewe akizungumza na kushirikiana nawe.
Bwana ameweka moyoni mwangu kuwa na Ujumbe Maalum na Ibada ya Ushirika katika Mkesha wa Mwaka Mpya tena mwaka huu. Ni jambo gani kubwa zaidi tunaloweza kufanya, Enyi marafiki, kuliko kuisikia Sauti ya Mungu ikizungumza nasi, kushiriki Meza ya Bwana, na kuyaweka wakfu tena maisha yetu kwa huduma Yake wakati wa kuukaribisha Mwaka Mpya. Utakuwa wakati mtakatifu jinsi gani kuufungia nje ulimwengu, na kuungana na Bibi-arusi kwa ajili ya huku kukusanyika Maalum katika Neno, tunaposema kutoka mioyoni mwetu, “Bwana, utusamehe makosa yote tuliyofanya mwaka mzima; sasa tunakukaribia Wewe, tukikuomba ikiwa utatushika mkono na kutuongoza mwaka huu ujao. Jalia tukutumikie Wewe zaidi ya tulivyowahi, na kama ni katika Mapenzi Yako ya Kiungu, jalia uwe ndio mwaka wa ule Unyakuo mkuu utakaotukia. Bwana, tunataka tu kwenda Nyumbani kuishi Nawe Milele yote.” Nasubiri kwa hamu kukusanyika kukizunguka Kiti Chake cha Enzi kwa ajili ya ibada hii maalum ya kujiweka wakfu upya, Bwana asifiwe.
Kwa waamini walio katika eneo la Jeffersonville, ningependa kuianza kanda saa 1:00 MOJA JIONI katika saa za eneo letu. Ujumbe kamili na ibada ya Ushirika itakuwa kwenye Redio ya Sauti wakati huo, kama tulivyofanya wakati uliopita. Vifurushi vya divai ya Ushirika vtapatikana Jumatano, tarehe 18 Desemba, kuanzia 7:00 – 11:00 jioni, kwa wewe kuja kuchukua kwenye jengo la YFYC.
Kwa wale ambao wanaishi nje ya eneo la Jeffersonville, tafadhali iweni na ibada hii maalum kwa wakati unaofaa kwenu. Tutakuwa na anuani ya kupakuliwa yenye Ujumbe na Ushirika hivi karibuni.
Tunapokaribia Sikukuu ya Krismasi, nataka nikutakie wewe na familia yako Msimu wa AJABU na SALAMA wa Sikukuu, na KRISmasi Njema, iliyojaa furaha ya Bwana Yesu aliyefufuka…Lile NENO.
Mpendwa Bibi-arusi wa Kanisa la Nyumbani, hebu sote tukusanyike pamoja na kuusikia Ujumbe 60-1218 Sauti Isiyojulikana, Jumapili hii saa 12:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville.( Ni saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki)
Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti Yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja Nami.
Enyi wahudumu, mfungulieni milango yenu malaika wa Mungu kabla hamjachelewa. Irudisheni Sauti ya Mungu kwenye mimbara zenu kwa kuzicheza kanda. Ndiyo Sauti pekee ya Mungu iliyothibitishwa kwa ajili ya siku yetu yenye Maneno ya kutokosea. Ndiyo Sauti pekee yenye Bwana Asema Hivi. Ndiyo Sauti pekee ambayo Bibi-arusi wote wanaweza kusema AMINA kwake.
Huu ndio wakati mkuu wa nyakati zote. Yesu anatupa sifa Yake kwa vile siku za neema Yake zinakwisha. Wakati umefika mwisho. Ametufunulia tabia Zake hasa katika wakati huu wa mwisho. Yeye ametupa mtazamo mmoja wa mwisho wa Uungu Wake mkuu wa neema. Wakati huu ni ufunuo wa jiwe la kifuniko wa nafsi Yake.
Mungu alikuja katika wakati huu wa Laodikia na kunena kupitia mwili wa mwanadamu. Sauti Yake imerekodiwa na kuhifadhiwa ili kumwongoza na kumkamilisha Bibi-arusi Neno Wake. Hakuna kabisa Sauti nyingine inayoweza kumkamilisha Bibi-arusi Wake ila Sauti Yake Mwenyewe.
Katika wakati huu wa mwisho, Sauti Yake iliyo kwenye kanda imewekwa kando; imetolewa nje ya makanisa. Hawataki tu kabisa kuzicheza kanda. Kwa hiyo Mungu anasema, “Mimi niko kinyume nanyi nyote. Nitawatapika mtoke katika kinywa Changu. Huu ni mwisho.”
“Kwa kuwa saba kati ya nyakati saba, sijaona kitu ila watu wakiliheshimu neno lao wenyewe kuliko Langu. Kwa hiyo mwishoni mwa wakati huu ninawatapika mtoke katika kinywa Changu. Yote yamekwisha. Nitazungumza basi. Naam, niko hapa katikati ya Kanisa. Amina wa Mungu, aliye mwaminifu na wa kweli atajifunua Mwenyewe na itakuwa KWA NJIA YA NABII WANGU.”
Kama ilivyokuwa hapo awali, wao wanafanya vile vile walivyofanya baba zao katika siku za Ahabu. Kulikuwa na jumla yao mia nne na wote walikubaliana; na wote wakisema jambo lile lile, waliwadanganya watu. Lakini nabii MMOJA, MMOJA TU, alikuwa sahihi na hao wengine wote walikuwa makosani kwa sababu Mungu alikuwa ametoa ufunuo kwa MMOJA TU.
Hii si kusema kwamba huduma zote ni za uongo na zinawadanganya watu. Wala Mimi sisemi mtu mwenye wito wa kuhudumu hawezi kuhubiri au kufundisha. Ninasema huduma tano ya KWELI itaweka KANDA, Sauti ya Mungu kwa Bibi-arusi, kuwa ndio Sauti iliyo muhimu sana UNAYOPASWA KUISIKIA. Sauti iliyo kwenye kanda ndio Sauti PEKEE ambayo imethibitishwa na Mungu Mwenyewe kuwa Bwana Asema Hivi.
Jihadharini na manabii wa uongo, kwa maana wao ni mbwa mwitu wakali.
Utajuaje kwa hakika njia sahihi kwa ajili ya siku hii? Kuna mgawanyiko jinsi hii miongoni mwa waaminio. Kundi moja la watu linasema huduma tano itamkamilisha Bibi-arusi, huku jingine linasema Bonyeza Play tu. Hatupaswi kugawanyika; tunapaswa kuungana kama BIBI-ARUSI MMOJA. Jibu sahihi ni lipi?
Hebu na tuifungue mioyo yetu pamoja na tusikie kile Mungu anachosema kwa Bibi-arusi kupitia nabii Wake. Kwa maana sote tunakubali, Ndugu Branham ndiye malaika-mjumbe Wake wa saba.
Juu ya msingi wa tabia za wanadamu peke yake, mtu ye yote anajua ya kwamba palipo na watu wengi kuna hata na maoni yasiyopatana juu ya mambo madogo-madogo ya fundisho muhimu ambalo wote wanashikilia pamoja. Ni nani basi atakayekuwa na mamlaka ya kutokosea ambayo itarudishwa katika wakati huu wa mwisho, kwa kuwa wakati huu wa mwisho utarudi kwenye kumdhihirisha Bibi-arusi wa Neno Halisi? Hiyo inamaanisha tutakuwa na Neno tena kama lilivyotolewa kikamilifu, na kueleweka kikamilifu katika siku za Paulo. Nitakwambia ni nani atakayekuwa nalo. Itakuwa ni nabii aliyethibitishwa kinaganaga, ama hata aliyethibitishwa kinaganaga zaidi kuliko nabii ye yote katika nyakati zote tangu Henoko hata siku hii, kwa sababu mtu huyu itambidi kuwa na huduma ya kinabii ya jiwe la kifuniko, na Mungu atamtambulisha. Haitambidi kujitetea, Mungu atamtetea kwa sauti ya ishara. Amina.
Hivyo, Ujumbe huu ulionenwa na mjumbe Wake ulitolewa kikamilifu, na unaeleweka kikamilifu.
Ni kitu gani kingine ambacho Mungu alichosema kumhusu malaika-mjumbe Wake wa saba na Ujumbe wake?
. Yeye atasikia tu kutoka kwa Mungu.
. Atakuwa na “Bwana asema hivi” na kunena kwa niaba ya Mungu.
. Yeye atakuwa kinywa cha Mungu.
. YEYE, KAMA INAVYOTANGAZWA KATIKA MALAKI 4:6, ATAIGEUZA MIOYO WA WATOTO IWAELEKEE BABA ZAO.
. Ata warudisha wateule wa siku za mwisho nao watamsikiliza nabii aliyethibitishwa akitoa kweli halisi kama vile ilivyokuwa kwa Paulo.
. Ata irudisha kweli kama walivyokuwa nayo.
Na kisha Yeye alisema nini kutuhusu sisi?
Na hao wateule walio pamoja naye katika siku hiyo watakuwa ndio wanaomdhihirisha Bwana kwa kweli na watakuwa ndio Mwili Wake na kuwa sauti Yake na kutenda kazi Zake. Haleluya! Unaliona hilo?
Kama ungali una mashaka yo yote juu ya jambo hili mwombe Mungu kwa Roho Wake akujaze na kukuongoza, kwa kuwa Neno linasema, “KWA MAANA WALIO WATEULE HAWAWEZI KUPUMBAZWA”. Hakuna mtu anayeweza kukupumbaza kama wewe ni Bibi-arusi.
Wakati Wamethodisti waliposhindwa, Mungu aliwainua wengine na kwa hiyo jambo hilo limeendelea kwa miaka mingi mpaka katika wakati huu wa mwisho kuna watu wengine nchini, ambao chini ya mjumbe wao watakuwa ndio sauti ya mwisho kwa wakati wa mwisho.
Naam bwana. Kanisa si “kinywa” cha Mungu tena. Ni kinywa chake lenyewe. Kwa hiyo Mungu analiacha. Ataliangamiza kupitia kwa nabii na bibi-arusi, kwa kuwa sauti ya Mungu itakuwa ndani ya bibi-arusi. Naam iko, kwa maana inasema katika sura ya mwisho ya Ufu. aya ya 17 “Roho na bibi-arusi wasema, njoo.” Mara nyingine tena ulimwengu utasikia moja kwa moja kutoka kwa Mungu kama ilivyokuwa wakati wa Pentekoste; lakini bila shaka huyo Bibi-arusi Neno atakataliwa kama ilivyokuwa katika wakati wa kwanza.
Bibi-arusi anayo sauti, bali itasema tu kile kilicho kwenye kanda. Kwa maana Sauti hiyo INATOKA MOJA KWA MOJA KWA MUNGU, hivyo haihitaji kufasiriwa kwa vile ilivyotolewa kikamilifu na inaeleweka kikamilifu.
Njoo uungane nasi Jumapili hii saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,(Ni Saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki) tunapoisikia Sauti hiyo ikitufunulia: Wakati wa Kanisa la Laodikia 60-1211E.
Haijawahi kutokea katika historia ya ulimwengu kuwepo na wakati ambapo Bibi-arusi wa Kristo kutoka ulimwenguni kote angeweza kuungana pamoja katika nia moja, wakati sauti kutoka Mbinguni, ile Sauti halisi ya Mungu, ingeweza kuja ikienda kasi.
Maandiko yanatimia. Ni ishara ya Mbegu ya wakati wa kuungana. Ule muungano usioonekana wa Bibi-arusi wa Kristo unafanyika tukiketi katika uwepo wa Mwana, tukiivishwa, tukijiweka wenyewe tayari kwa kuisikia Sauti ya Mungu halisi.
Sisi tunakamilishwa na huduma tano Yake.
Ni wangapi wanaoamini kwamba karama na miito havina majuto? Biblia ilisema kuna karama tano katika kanisa. Mungu ameweka katika kanisa Mitume, au wamishenari, mitume, manabii, waalimu, wainjilisti, wachungaji.
. Mhubiri: Ningeenda barabarani. Mtu fulani angesema, “Je, wewe ni mhubiri?” Ningesema, “Ndiyo bwana. Loo, Ndiyo, mimi ni mhubiri.”
. Mwalimu: Na sasa sababu sikuchukua kuhubiri asubuhi ya leo, ilikuwa ni kwamba, nilifikiri, katika kufundisha, tungelielewa vizuri zaidi kuliko kuchukua somo na kulipitia juu juu. Tungelifundisha tu.
. Mtume: Neno “mmishenari” linamaanisha “mtu aliyetumwa.” “Mtume” maana yake ni “mtu aliyetumwa.” Mmishenari ni mtume. Mimi—mimi, mimi ni mmishenari, kama mjuavyo, ninafanya uinjilisti, kazi ya kimishenari, karibu mara saba nchi za ng’ambo, kote ulimwenguni.
. Nabii: Je, unaniamini mimi kuwa nabii wa Mungu? Basi nenda ukafanye kile ninachokuambia.
. Mchungaji: Je, mumeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mumeniita “mchungaji wenu”; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo.
Nami nikawaona hao mamilioni wamesimama pale, nikasema, “Hivi hawa wote ni wa Branham?” Kasema, “La.” Kasema, “Hao ni waongofu wako.” Ndipo nikasema, ni—nikasema, “Ninataka kumwona Yesu.” Akasema, “Bado. Itachukua muda kabla Yeye hajaja. Ila atakuja kwako kwanza nawe utahukumiwa kwa Neno ambalo ulihubiri,
Ndipo sisi sote tutainua mikono yetu na kusema, “Tunatumainia hilo!”
Jambo fulani liko karibu kutukia. Nini kinatendeka? Waliokufa katika Kristo wameanza kufufuka pande zote kunizunguka. Ninahisi badiliko likija mwilini mwangu. Nywele zangu za mvi, zimeondoka. Angalia uso wangu… makunyanzi yangu yote yametoweka. Kuugua kwangu na maumivu…. YAMEKWISHA. Kuhisi kwangu huzuni kumetoweka mara moja. Nimebadilishwa kwa dakika moja, katika kufumba na kufumbua jicho.
Kisha tutaanza kutazama kando yetu na kuwaona wapendwa wetu. Loo, yule pale Mama na Baba…Utukufu, mwanangu…binti yangu. Babu, Bibi, loo, nimewakumbuka sana nyote wawili. Halo …yule pale rafiki yangu wa zamani. LOO, TAZAMA, ni Ndugu Branham, nabii wetu, Haleluya!! yuko hapa. Linatukia!
Kisha pamoja, wote kwa pamoja, tutanyakuliwa huko juu mahali fulani hewani ng’ambo ya nchi. Tutamlaki Bwana wakati akishuka. Tutasimama huko pamoja Naye juu ya mizingo ya dunia hii na kuziimba nyimbo za ukombozi. Tutaimba na kumsifu Yeye kwa ajili ya neema Yake ya ukombozi ambayo ametupa.
Ni mangapi yote yanayomngojea Bibi-arusi Wake. Tutakuwa na wakati ulioje katika umilele sisi kwa sisi, na pamoja na Bwana wetu Yesu. Maneno ya kibinadamu hayawezi kueleza, Bwana, jinsi tunavyojisikia mioyoni mwetu.
Kama ungependa kumsikia Yeye akikuita Bibi-arusi Wake, na kukuambia jinsi gani itakavyokuwa pamoja Naye, njoo uungane nasi Jumapili hii saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,(Ni Saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki), nawe utabarikiwa kupita kipimo.
Ndugu. Joseph Branham
60-1211M Wale Wanawali Kumi, Na Wayahudi Mia Na Arobaini na Nne Elfu
Je! Jumapili hii itashikilia kitu gani kwa ajili ya Bibi-arusi wa Yesu Kristo? Ni yapi yote Roho Mtakatifu atakayotufunulia? Utimilifu Mkamilifu. Sasa tutafahamu kikamilifu kwa Ufunuo, kitu chenyewe ukilinganisha na mfano wake na kitu chenyewe na kivuli chake. Yesu ndiye mkate wa kweli wa Uzima. Yeye ndiye wote wa Hilo. Yeye ni Mungu Mmoja. Yeye ni Waebrania 13:8. Yeye ndiye MIMI NIKO.
Kristo, akiisha kutokea katika mwili na kumwaga Damu Yake mwenyewe, ameziondoa dhambi zetu mara moja na kwa yote kwa toleo la nafsi Yake; kwa hiyo sasa ametufanya sisi kuwa WAKAMILIFU. Uhai Wake mwenyewe umo ndani yetu. Damu Yake imetusafisha. Roho Wake hutujaza. Mapigo Yake TAYARI yametuponya. Neno Lake liko ndani ya mioyo na mdomo wetu. Ni Kristo katika maisha yetu na si kitu kingine chochote, kwani kila kitu maishani mwetu hufifia na kuwa duni, isipokuwa Yeye na Neno Lake.
Mioyo yetu itajawa na furaha anapotuambia kwamba kwa uamuzi wa kiungu, Yeye alijua ni nani hasa angalikuwa Bibi-arusi Wake. Jinsi alivyotuchagua. Yeye alituita. Alitufia sisi. Alitununua na sisi ni mali Yake, na ni Wake peke Yake. Yeye hunena, nasi tunatii, kwa maana hiyo ndiyo furaha yetu. Sisi ni mali Yake peke Yake Naye hana mwingine ila SISI. Yeye ni Mfalme wetu wa Wafalme nasi ni ufalme Wake. Sisi ni mali Yake ya milele.
Yeye atatutia nguvu na kutuangazia kwa Neno la Sauti Yake. Ataeleza waziwazi na kufunua kuwa Yeye ndiye Mlango wa kondoo. Yeye ni Alfa na Omega. Yeye ni Baba, Yeye ni Mwana, na Yeye ni Roho Mtakatifu. Yeye ni Mmoja, nasi tu Mmoja na Naye na ndani Yake.
Yeye atatufundisha subira, kama alivyomfundisha Ibrahimu, kwa kueleza jinsi tunavyopaswa kungojea kwa subira na kuvumilia ikiwa tunataka kupata ahadi yoyote.
Yeye atatuonyesha waziwazi siku hasa tunayoishi. Jinsi zile pilikapilika za ekumeni zitakavyopata nguvu kisiasa, na kuishurutisha serikali kuwafanya wote waungane nao aidha moja kwa moja ama kwa kufuata kanuni zilizofanywa sheria hivi kwamba hakuna watu watakaotambuliwa kama makanisa isipokuwa chini ya uongozi wa moja kwa moja ama usio wa moja kwa moja wa halmashauri yao.
Yeye atafunua jinsi gani wengi sana watakubaliana nao, wakidhani wanamtumikia Mungu katika utaratibu uliowekwa wa shirika. Bali Yeye anatuambia sisi, “Msiogope, kwa maana Bibi-arusi hatadanganywa, sisi tutadumu na Neno Lake, Sauti Yake.”
Litakuwa jambo lakutia moyo jinsi gani kumsikia Yeye akituambia: “Shika sana, vumilia. Usife moyo, bali vaa silaha zote za Mungu, kila silaha, kila karama niliyokupa iko mikononi mwetu. Usivunjike moyo kamwe kipenzi, endelea tu kuangalia mbele kwa furaha kwa sababu utatiwa taji na Mimi, Mfalme wako wa Wafalme na Bwana wa Mabwana, Mumeo.”
Ninyi ndio kanisa Langu la kweli; hekalu halisi la Mungu kwa Roho Wangu Mtakatifu aishiye ndani yenu. Mtakuwa nguzo katika hilo hekalu jipya; ule msingi utakaoshikilia sehemu ya juu. Nitawaweka kama washindi pamoja na mitume na manabii, kwa maana Nimewapa Ufunuo wa Neno Langu, wa Mimi Mwenyewe.
Yeye atatufunulia waziwazi kwamba majina yetu yaliandikwa katika Kitabu Chake cha Uzima cha Mwana-Kondoo kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa hiyo tutakuwa mbele ya kiti Chake cha enzi usiku na mchana kumtumikia hekaluni Mwake. Sisi tuko chini ya ulinzi maalum wa Bwana; sisi ni Bibi-arusi Wake.
Tutakuwa na jina jipya kwa kulichukua jina Lake. Litakuwa ndilo jina tulilopewa sisi wakati anapotuchukua Kwake. Tutakuwa Bi Yesu Kristo Wake.
Yerusalemu mpya ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, Bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa Mumewe. Mauti haitakuwapo tena, huzuni, wala kilio. Wala maumivu hayatakuwapo tena kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Ahadi zote nzuri za Mungu zitatimizwa. Badiliko litakamilika. Mwana-Kondoo na Bibi-arusi Wake watakaa milele katika ukamilifu wote wa Mungu.
Mpendwa Bi Yesu Kristo, OTA JUU YAKE. Itakuwa nzuri zaidi kuliko vile unavyoweza kuwazia.
Ninamwalika kila mtu aje kuungana nasi Jumapili hii saa 6:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,( saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki ) wakati Mume wetu, Yesu Kristo, anenapo kupitia malaika-mjumbe Wake wa saba mwenye nguvu na kutuambia mambo haya yote.
Tunajivunia jinsi gani kuitwa “Watu wa Kanda”. Mioyo yetu inaenda mbio kwa changamko kila wiki tukijua tutaungana pamoja ulimwenguni kote kwa kuisikia Sauti ya Mungu ikisema nasi.
Tunajua, bila chembe ya shaka hata moja, tuko katika Mapenzi makamilifu ya Mungu kwa sisi kukaa na Neno Lake; kuisikiliza Sauti Yake kwa njia ya malaika-mjumbe Wake wa saba mwenye nguvu.
Mjumbe Aliyemchagua kwa ajili ya siku yetu ni William Marrion Branham. Yeye ndiye taa ya Mungu kwa ulimwengu, inayoakisi nuru ya Mungu. Yeye anamwita Bibi-arusi Neno Safi Wake aliyechaguliwa atoke kupitia malaika Wake.
Kwa kujifunza kwa makini Neno Lake, Ametufunulia sisi kwa Roho Wake Mtakatifu kwamba William Marrion Branham ndiye malaika ambaye Yeye aliyemchagua kumpa Ufunuo Wake na Huduma Yake kwa ajili ya siku yetu. Tunamwona malaika Wake, NYOTA YETU, katika mkono Wake wa kuume huku akimpa nguvu Zake za kufunua Neno Lake na kumwita Bibi-arusi Wake atoke.
Yeye ametupa Ufunuo mzima wa Yeye Mwenyewe. Roho Mtakatifu akijitambulisha kwetu kupitia maisha ya malaika-mjumbe Wake wa saba; malaika aliyemchagua kuwa macho Yake kwa ajili ya siku yetu.
Jinsi gani mioyo yetu inavyowaka ndani yetu wakati anapotuambia kwa kila Ujumbe kwamba ni kusudi Lake kutuleta Kwake; ya kwamba sisi ni Bibi-arusi Neno Wake.
Yeye anapenda kutuambia mara kwa mara jinsi alivyotuchagua sisi kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu NDANI YAKE. Jinsi tulivyojulikana kimbele na kupendwa Naye.
Jinsi tunavyopenda kumsikia Yeye akinena na kutuambia tulikombolewa kwa Damu Yake na HATUWEZI kamwe kuja hukumuni. Hatuwezi kamwe kuwa katika hukumu, kwa sababu dhambi haiwezi kuhesabiwa kwetu sisi.
Jinsi tutakavyoketi pamoja Na Yeye wakati akichukua kiti chake cha enzi cha duniani cha Daudi, na kutawala pamoja Naye; kama tu Yeye alivyofanya mbinguni, pamoja na uwezo na mamlaka juu ya dunia nzima. Majaribu na majaribio ya maisha haya yataonekana kuwa si kitu wakati huo.
Lakini pia Yeye ametuonya jinsi gani tunavyopaswa kuwa waangalifu. Kwamba katika nyakati zote ile mizabibu miwili ilikua pamoja. Jinsi ambavyo adui daima amekuwa akifanana sana; mdanganyifu sana. Hata Yuda alichaguliwa na Mungu, na kufundishwa katika kweli. Alishiriki maarifa ya zile siri. Alikuwa na huduma ya nguvu aliyopewa naye akawaponya wagonjwa na kutoa pepo katika Jina la Yesu. Lakini yeye hakuweza kwenda hadi mwisho.
Huwezi kuendelea na sehemu tu ya Neno, huna budi kuchukua Neno LOTE. Kuna watu wanaoonekana wanahusika na mambo ya Mungu karibu asilimia mia moja, lakini sio.
Yeye alisema wala haitoshi kwamba Yeye amejihusisha na kanisa zima, ama hata na huduma tano ya Waefeso nne. Yeye alituonya kwamba katika kila wakati kanisa hupotoka, na wala si wafuasi tu bali na kundi la makasisi – wachungaji wako makosani na kondoo pia.
Kwa hiyo kwa shauri lililokusudiwa la mapenzi Yake Mwenyewe, Yeye amejitokeza Mwenyewe katika wakati wetu kama Mchungaji Mkuu katika huduma ya malaika-mjumbe Wake wa saba kuwaongoza watu Wake wairudie ile kweli na zile nguvu nyingi za kweli hiyo.
Yeye yuko ndani ya mjumbe Wake na yeye ambaye angekuwa na utimilifu wa Mungu angemfuata huyo mjumbe kama vile huyo mjumbe alivyo mfuasi wa Bwana kwa Neno Lake.
Ninataka kuwa na utimilifu wa Mungu na kumfuata mjumbe Wake. Hivyo, kwetu sisi, Maskani ya Branham, njia pekee ya kumfuata mjumbe kama vile yeye anavyomfuata Bwana kwa Neno Lake, ni KUBONYEZA PLAY na kuisikia Sauti ya Mungu Safi ikisema nasi maneno ya kutoweza kukosea.
Haitubidi kukisia au kukagua kile tunachosikia, inatubidi tu Kubonyeza Play na kuamini kila Neno tunalosikia.
Nilimsikia Ndugu Branham akisema maneno yafuatayo mapema asubuhi moja kwenye redio ya Sauti. Nilipolisikia Hilo, ikanijia moyoni mwangu kwamba hivi ndivyo Mimi / sisi tunavyojisikia kuhusu kusema:
TUNABONYEZA PLAY TU NA KUZISIKILIZA KANDA.
Ilisikika kama tamshi la Imani yetu kwangu mimi.
Hiyo ndiyo sababu ninaamini katika uponyaji wa Kiungu. Hiyo ndiyo sababu ninaamini katika maono. Hiyo ndiyo sababu ninaamini katika Malaika. Hiyo ndiyo sababu ninaamini Ujumbe huu, ni kwa sababu unatoka kwenye Neno la Mungu. Na chochote nje ya Neno la Mungu, sikiamini. Inaweza kuwa hivyo, lakini hata hivyo nitadumu tu na yale Mungu aliyosema, ndipo niwe na hakika kwamba niko sahihi. Sasa, Mungu anaweza kufanya atakalo. Yeye ni Mungu. Lakini maadamu ninadumu na Neno Lake, basi ninajua hilo ni sawa. Ninaamini hilo.
Utukufu, yeye alilisema KAMILIFU kweli. Huduma zingine zote zinaweza kuwa, kwa sababu Mungu anaweza kufanya atakalo, na yule Yeye anayemtaka kulifanya, Yeye ni Mungu. Lakini maadamu ninadumu na Neno Lake, Sauti Yake, Kanda, basi ninajua hilo ni sawa. Ninaamini hilo.
Ninajua wengi huzisoma barua zangu na kutoelewa kile Mimi ninachosema na kile ninachoamini kuwa ni Mapenzi ya Bwana kwa kanisa letu. Nami niseme tena kwa unyenyekevu kama vile nabii alivyosema: “Barua hizi zimekusudiwa kwa ajili ya kanisa langu peke yake. Wale wanaotamani kuiita Maskani ya Branham kanisa lao. Wale WANAOTAKA KUTAMBULISHWA NA KUITWA WATU WA KANDA”.
Ikiwa hukubaliani na yale ninayosema na ninayoamini, hiyo ni sawa asilimia 100% ndugu zangu na dada zangu. Barua zangu si kwa ajili yenu au dhidi yenu au kwa makanisa yenu. Kanisa lako linajitawala lenyewe nawe ni lazima ufanye kama vile unavyohisi kuongozwa kufanya, bali kulingana na Neno, ndivyo lilivyo na letu, na hiki ndicho sisi tunachoamini kuwa ndio njia iliyoandaliwa na Mungu kwa ajili yetu.
Wote mnakaribishwa kuungana nasi kila Jumapili saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville.( Ni Saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki ) Wiki hii, Nyota ya Mungu ya wakati wetu, William Marrion Branham, atakuwa akituletea Ujumbe, 60-1209 Wakati wa Kanisa la Sardi.
Jinsi ambavyo Bwana anavyotufunulia kwamba katika nyakati zote kumekuwa na kundi dogo sana ambalo lilidumu na Neno Lake. Wao hawakuanguka katika mtego wa udanganyifu wa adui, bali walibaki wa kweli na waaminifu kwa Neno la siku yao.
Lakini hakujawahi kuwa na wakati, au kundi la watu, ambalo Bwana amekuwa akijivunia, au kuwa na imani zaidi nalo, kuliko sisi. Sisi ndio Bibi-arusi Bibi Mteule Wake ambaye hatadanganywa, na hata muhimu zaidi HATUWEZI, kudanganywa; kwa maana sisi tunaisikia Sauti ya Mchungaji na kumfuata.
Yeye anatuonyesha kwamba katika nyakati zote kumekuwa na makundi mawili ya watu, yote yakidai ufunuo wao kutoka kwa Mungu na uhusiano wao na Mungu. Lakini alituambia, Bwana awajua walio Wake. Anafuatilia mawazo yetu. Yeye anajua kilicho mioyoni mwetu. Yeye anaziona kazi zetu kwa kudumu na nabii na Neno Lake, ambayo ni madhihirisho dhahiri ya yale yaliyo ndani yetu. Madhumuni yetu, makusudi yetu yanajulikana Kwake kwa kuwa Yeye hulichunguza kila tendo letu.
Yeye anatuambia kwamba ahadi zote alizozitoa kwa kila wakati, ni ZETU. Anatuona sisi tunaoendelea kutenda kazi Zake kwa uaminifu hata mwisho. Yeye AMETUPA SISI mamlaka juu ya mataifa. Anatuambia sisi ni viongozi wenye nguvu, hodari, shupavu ambao wanaweza kukabiliana vizuri sana na hali yo yote. Hata adui aliye mbaya sana atavunjwa kama kukiweko na haja. Dhihirisho letu la kutawala kwa mamlaka Yake litakuwa kama lile lile la Mwanawe. UTUKUFU!!
Tumepata ujuzi wa kina cha Mungu katika maisha yetu. Ni tukio la kibinafsi la Roho wa Mungu akiishi ndani yetu. Nia zetu zinaangazwa na hekima na maarifa ya Mungu kwa kupitia Neno Lake.
Sisi tunaenda po pote Bwana-arusi alipo. Hatutaachwa Naye kamwe. Hatutaondoka ubavuni Mwake. Tutashiriki kiti cha enzi pamoja Naye. Tutatiwa taji kwa utukufu na sifa Zake.
Yeye ametufunulia jinsi gani ambavyo adui amekuwa mdanganyifu katika kila wakati na jinsi ilivyo muhimu KUDUMU NA NENO LAKE LA ASILI. Hakuna Neno moja linaloweza kubadilishwa. Kila wakati waliongeza kwake na kuondoa kutoka kwake, wakiweka fasiri yao wenyewe kwenye Neno la asili; nao wanapotea milele kwa kufanya hivyo.
Katika Wakati wa Kanisa la Thiatira, hiyo roho ya udanganyifu ilinena kupitia papa wa Rumi na kulibadilisha Neno Lake. Alilifanya kuwa “mpatanishi mmoja kati ya Mungu na mwanadamu (si wanadamu).” Kwa hiyo sasa yeye anapatanisha kati ya mpatanishi na wanadamu. Hivyo, mpango wote wa Mungu ulibadilishwa; si kwa kubadili neno, bali kwa kubadili HERUFI MOJA. Shetani alikuwa amebadilisha “E” kuwa “A”.
Kila Neno litahukumiwa kwa Neno Lake la Asili lililonenwa kwenye kanda. Kwa hiyo, Bibi-arusi Wake LAZIMA adumu na kanda. Wakati adui anajaribu kuwakatisha tamaa watu kwa kuwapa mpango tofauti, wazo tofauti, herufi tofauti, Bibi-arusi ATADUMU NA NENO LA ASILI.
Katika kila wakati Yesu anajitambulisha Mwenyewe na mjumbe wa wakati huo. Wao wanapokea kutoka Kwake ufunuo juu ya Neno kwa ajili ya wakati wao. Ufunuo huu wa Neno huwaleta wateule wa Mungu kutoka katika ulimwengu na waingie katika muungano mkamilifu na Yesu Kristo.
Yeye amewaita na kuwaweka wakfu watu wengi ili wawe baraka kwa kanisa, lakini Yeye ana ila MJUMBE MMOJA TU ambaye Yeye alimuita ili KULIONGOZA kanisa Lake kwa Roho Wake Mtakatifu. Kuna SAUTI MOJA yenye Bwana Asema Hivi. Kuna SAUTI MOJA ambayo Yeye alisema atatuhukumu kwayo. Kuna SAUTI MOJA ambayo Bibi-arusi Wake wameweka kikomo chao cha Milele. SAUTI HIYO NI SAUTI YA MUNGU ILIYO KWENYE KANDA.
Bibi-arusi, Mapenzi ya Mungu kwetu ni Ukamilifu, na mbele zake, sisi NI WAKAMILIFU. Na huo ukamilifu ni subira, kumngojea Mungu… na kumngoja Mungu. Anatuambia ni njia ya kuumba tabia zetu. Tunaweza kuwa na mitihani, majaribu na dhiki nyingi, lakini uaminifu wako kwa Neno Lake unafanya subira ndani yetu ili tuwe wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa na neno.
Hatutasahau kamwe IMANI huja kwa kusikia, kusikia Neno, nalo Neno huja kwa nabii.
Njoo ujionee furaha kuu ya maisha yako unapoketi pamoja nasi katika Mahali pa Mbinguni tunapoisikia Sauti ya Mungu ikituletea Neno juu ya: Wakati wa Kanisa la Thiatira 60-1208, saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville.(Ni Saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki)
Je! Mmekuwa mkifurahia Nyakati Saba za Kanisa? Mungu anampa Bibi-arusi Wake ufufuo kuliko hapo awali. Yeye anatupa Ufunuo zaidi, Imani zaidi, na hakikisho zaidi kujua sisi ni nani, na kile tunachofanya kwa kukaa na Neno, Njia Yake aliyoiandaa kwa ajili ya siku hii.
Sasa Yeye anatuambia: “Kuanzia ibada ya Jumapili na kuendelea, vaeni mawazo yenu ya kiroho. Acha Roho Mtakatifu alizamishe Hilo ndani na myashike matumizi ya kiroho katika yote nitakayofanya. Ni Neno Langu lililohuishwa na Roho lililonenwa na nabii Wangu wa Malaki 4.”
Hebu na tusome na tuyapate machache ya Maneno Yake nasi tutumie mawazo yetu ya kiroho kuyahusu.
Mungu alimweka kiongozi Wake aliyejazwa Roho kwa ajili ya kundi Lake lililojazwa na Roho; malaika Wake; Naye akatia juu yake muhuri wa jina, bali haimpasi kulifunua. Hapaswi kumwambia mtu, mnaona. “Hakuna mtu ajuaye ila yeye mwenyewe.”
Kwa hiyo Mungu alimpa Bibi-arusi Wake kiongozi aliyejazwa na Roho kwa ajili ya kundi Lake lililojazwa na Roho. KIONGOZI, SIO VIONGOZI kwa ajili ya kundi Lake lililojazwa na Roho.
Anayekuja ulimwenguni hivi karibuni, yule malaika mkuu wa Nuru atakayetujia, atakayetuongoza tutoke, Roho Mtakatifu mkuu, akija mamlakani, naye atatuongoza kwa Bwana Yesu Kristo.
Malaika mkuu wa Nuru. Malaika mkuu wa Nuru ni nani kwa wakati huu wa mwisho? William Marrion Branham. Yeye hazungumzi juu ya Roho Mtakatifu. Yeye tayari amekwishakuja naye anasema atakayekuja.
Atakaye TUONGOZA TUTOKE. Kwa kweli tunajua na kuamini kwamba ni Roho Mtakatifu anayetuongoza, lakini Yeye ameweka wazi malaika Wake na Roho Mtakatifu pamoja na kusema Yeye (Roho Mtakatifu Wake) atakuwa akituongoza (KUPITIA) malaika Wake mkuu wa Nuru.
Yeye anaendelea kuwaunganisha pamoja kwa kusema:
Labda hatajua hilo,
Yeye hasemi Roho Mtakatifu hatamjua ni nani, bali malaika-mjumbe Wake wa duniani yule ambaye Yeye amemchagua KUTUONGOZA TUTOKE.
Bali atakuwa hapa moja ya siku hizi. Atafanya… Mungu atamtambulisha. Haitambidi kujitambulisha mwenyewe, Mungu atamtambulisha. Mungu atamthibitisha aliye Wake.
Tena, Yeye hasemi Roho Mtakatifu atakuwa hapa MOJA YA SIKU HIZI, bali malaika Wake mkuu wa Nuru ili kumwongoza Bibi-arusi Wake. Haitambidi kujitambulisha mwenyewe, Mungu atamtambulisha kiongozi Wake mkuu kwa Bibi-arusi Wake Mwenyewe kwa UFUNUO.
Je, umeyashika matumizi ya kiroho? Je! unaona malaika wa Nuru ni nani ambaye Mungu alimchagua kumwongoza Bibi-arusi Wake? Je! Inasema hapa ati kijiti kimepokezwa viongozi wengine?
Kamwe hutaweza kuishi juu zaidi ya mchungaji wako. Kumbuka hilo tu, unaona.
Ingawa wengine wanaweza wasituelewe na kutudhihaki, jinsi sisi tunavyofurahi na tunavyoshukuru kweli kwa Ufunuo kusema, WILLIAM MARRION BRANHAM NDIYE MCHUNGAJI WETU.
Sasa kwa kuwa kila moja ya jumbe hizi umeelekezwa kwa ‘malaika’—(mjumbe wa kibinadamu) wajibu mkubwa sana na pia majaliwa makuu sana ni fungu lake.
Ujumbe ulielekezwa kwa malaika Wake, kisha malaika Wake anampa huo Bibi-arusi; si wahudumu tu, bali kwa BIBI-ARUSI WAKE WOTE Nao upo kwenye kanda kwa wote kuusikia. Hauwezi kuongezwa kwake au kuondolewa kitu kwake, Nao HAUHITAJI FASIRI YO YOTE.
“Hivi karibuni Yeye atakuja. Na atakapokuja, Yeye atakuja kwako kwanza. Nawe utahukumiwa kulingana na Injili uliyohubiri, nasi tutakuwa raia wako.” Nikasema, “Wataka kusema ninawajibika kwa hawa wote?” Akasema, “Sisi sote. Wewe ulizaliwa kiongozi.”
Wakati siku ile kuu ya hukumu itakapokuja, Yeye anakuja kwanza kwa malaika Wake wa Nuru naye atamhukumu yeye kwanza kulingana na injili aliyohubiri. Sisi ni RAIA WAKE. Yeye anawajibika kwa kila mmoja wetu kwa kuwa yeye alikuwa KIONGOZI aliyechaguliwa na Mungu.
Weka matumizi yako ya kiroho kwenye jambo hilo. Tutahukumiwa kwa yale ambayo malaika wa Mungu aliyosema. Kwa hiyo, unataka kubahatisha kuhusu uzima wako wa milele kwa kile mtu fulani anachosema ALISEMA wakati wewe unaweza kusikia moja kwa moja kutoka KWAKE?
Anawezaje mtu yeyote kuamini kuwa kuna HUDUMA MUHIMU KULIKO ILE ILIYO KWENYE KANDA. Ikiwa unaamini hivyo, au umeshawishiwa hivyo kwa hoja, ni afadhali urudi kwenye NENO LA ASILI; kwa maana utahukumiwa kwa maneno yaliyo kwenye kanda. Dumu na Neno kama vile Lilivyonenwa.
Lakini huyu nabii atakuja, na kama vile yule mtangulizi wa kule kuja kwa kwanza alivyopaza sauti, “Tazama Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu,” vivyo hivyo bila shaka naye atapaza sauti, “Tazama Mwana-Kondoo wa Mungu anayekuja katika utukufu.” Atafanya jambo hili, kwa maana kama vile Yohana alivyokuwa mjumbe wa ile kweli kwa wateule, ndivyo alivyo na huyu mjumbe wa mwisho kwa wateule na kwa bibi-arusi aliyezaliwa kwa Neno.
Ni nani atakayetutambulisha kwa Bwana Yesu? Malaika Wake mkuu wa Nuru, William Marrion Branham.
Njoo uwe Bibi-arusi Bikira Safi pamoja nasi tunapomsikia malaika-mjumbe Wake mkuu akituletea Ufunuo zaidi, Jumapili saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,(Ni saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki) tunaposikia Ujumbe 60-1207 – “Wakati wa Kanisa la Pergamo.”
Kuna kundi moja tu la watu; kundi maalum sana la watu, ambao wanaweza kusikia yale Roho anayosema katika wakati huu wa mwisho. Ni kundi maalum ambalo limeupokea Ufunuo wa wakati huu. Kundi hilo ni la Mungu. Kundi lile ambalo haliwezi kusikia, si la Mungu.
Kundi ambalo linaweza, na linasikia yale Roho anayosema, linapokea Ufunuo wa Kweli. Sisi ndio hao walio na Roho wa Mungu. Sisi ndio hao waliozaliwa na Mungu na kubatizwa kwa Roho Mtakatifu. Sisi ndio Bibi-arusi Wake Aliyejazwa Roho ambaye ameupokea Ufunuo kwa ajili ya wakati wetu.
Inamaanisha nini kwetu sisi Kubonyeza Play? UFUNUO! Ni kusikia, kupokea na kukaa na Njia ya Mungu iliyoandaliwa kwa ajili ya siku hii. Sauti ya Mungu mwenyewe ikinena mdomo kwa sikio na Bibi-arusi Wake. Ni Roho Mtakatifu akizungumza na mioyo na nafsi zetu.
Tunajua Mungu huwatumia watu waliotiwa mafuta na Roho wake kunena, lakini hakuna mahali pengine pa kuisikia Bwana Asema Hivi isipokuwa kwa Kubonyeza Play na kuisikia SAUTI ya malaika wake wa saba, William Marrion Branham. Ndiyo Sauti pekee iliyothibitishwa na Roho Mtakatifu Mwenyewe. Yeye ndiye Sauti ya Mungu, nabii wa Mungu, mchungaji wa Mungu, kwetu sisi, na kwa ulimwengu mzima.
Wakati Yeye anaponena, sisi tunasema AMINA kwa kila Neno; kwa maana ni Mungu mwenyewe anayesema nasi. Neno Lake ndilo Neno pekee lisilohitaji kufasiriwa. Ni Mungu akitumia sauti yake kuongea na Bibi-arusi Wake.
Ni Mungu mwenyewe anayetuambia, “Watoto wangu, si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi. Kabla hakujawa na chembe ya vumbi ya nyota; kabla hata sijajulikana kwako kuwa Mungu wako, Nilikujua. Ulikuwa Niani Mwangu, ukiwa katika Mawazo Yangu ya milele. Wewe ni Bibi-arusi Wangu halisi wa Uzao Wa Neno Lililonenwa.
Ingawa mlikuwa katika Mawazo Yangu ya milele, Sikuwadhihirisha hadi majira Yangu niliyoyakusudia na yaliyoamriwa. Kwa maana nilijua NINYI mngekuwa kundi langu maalum ambalo lingedumu na Neno Langu. Wengine wote wameshindwa, lakini Nilijua ninyi hamgeshindwa.
Ninajua ya kwamba unateswa na kudhihakiwa kwa sababu umedumu na nabii Wangu, lakini wewe ndiye Mzabibu Wangu wa Kweli ambao haujakengeuka kutoka kwenye Neno Langu, bali umedumu kuwa mkweli na mwaminifu kwa nabii Wangu ambaye hunena Maneno Yangu.
Kuna wengine wengi ambao wamefundishwa kwa uaminifu, lakini wao daima hawajifunzi jinsi ilivyo jambo muhimu kusema yale tu Mimi Niliyoyanena kupitia mjumbe Wangu.”
Jinsi tunavyopaswa kuwa waangalifu kusikia sauti MOJA, kwa kuwa Roho hana ila sauti moja ambayo ni sauti ya Mungu.
Loo! jinsi ilivyo muhimu kusikia sauti ya Mungu kwa njia ya wajumbe Wake, halafu kusema yale waliyopewa kuyaambia makanisa.
“Neno Langu daima limemjia nabii Wangu, lakini katika siku hii, Ilinibidi niirekodi Sauti Yangu ili KUSIWEKO NA MAKOSA kwa yale niliyomwambia Bibi-arusi. Kuna timazi moja tu, fimbo moja tu, na hiyo ni NENO nililolinena Mimi kupitia malaika Wangu. Kama ilivyo katika kila wakati, nabii Wangu ndiye Neno la siku hiyo.”
Kanda, Sauti Yake, ni barua ya mahaba kwetu sisi. Wakati adui anapotupiga mara kwa mara kupitia majaribio na dhiki na shida zetu, Yeye alimtuma malaika Wake mwenye nguvu kutuambia kwamba si chochote ila upendo wa kuchagua wa Mungu kwetu sisi, akituthibitishia kwamba ametuchagua sisi kwani hatutaondoshwa.
Kusudi Lake kuu ni kwamba baada ya sisi kuteseka kwa muda kidogo, angetufanya wakamilifu, atuimarishe na kututia nguvu. Alituambia kwamba hata Bwana wetu Yesu alikamilishwa kwa mateso Yake. Ni baraka iliyoje ambayo Yeye ametuachia. Kwa maana kwa mateso yetu, Yeye angetufikisha katika ukamilifu pia.
Anatujenga tabia kupitia majaribio na dhiki zetu. Maana tabia yetu haiumbiki bila mateso. Hivyo, mateso yetu ni USHINDI kwetu, na si karama.
Tunawezaje kuuthibitisha upendo wetu Kwake?
¶ Kwa kuamini yale aliyosema.
¶ Kukaa na Neno Lake.
¶ Kuenenda kwa furaha katikati ya majaribio na dhiki zetu, ambayo Yeye, katika hekima Yake kuu, anayaruhusu yatimie.
Jinsi anavyoinua roho zetu kwa kulisikia Neno Lake. Sauti Yake hufariji nafsi zetu. Tunapobonyeza Play na kumsikia Yeye akinena, mizigo yetu yote inainuliwa. Hatuwezi hata kuanza kufikiria ni hazina gani ambazo zimewekwa kwa ajili yetu kupitia dhiki zetu zote.
Loo, Bibi-arusi wa Yesu Kristo, ninayo furaha jinsi gani kuwa Mmoja Wao pamoja na kila mmoja wenu. Ni furaha iliyoje moyoni mwangu kujua Yeye ametupa Ufunuo wa Neno Lake. Wakati anapotuambia zitafanana sana ingewapoteza walio wateule kama yamkini, Yeye ametupa UFUNUO WA KWELI.
Njoo, uingie katika Roho pamoja nasi Jumapili hii saa 06:00 sita MCHANA, saa za Jeffersonville,(Ni saa 1:00 moja JIONI ya Afrika Mashariki) tunapolisikia Neno kamilifu: 60-1206 – Wakati wa Kanisa la Smirna.