UJUMBE: 63-1124E Aina Tatu Za Waamini
Mpendwa Mwamini,
Jinsi inavyopendeza kusema, MIMI NI MWAMINI. Si wa kanuni za imani; Neno! Si wa madhehebu; Neno! Si wa kile anachosema mtu mwingine; bali kile lisemacho Neno!
Sisi hatuulizi kitu, tunaliamini tu. Haidhuru Linasikika namna gani ama lolote mtu ye yote asemalo juu yake, sisi ni waamini halisi. Tuna ufunuo wa kiroho wa Neno.
Tunaiona ile saa tunayoishi. Tunauona ule Ujumbe wa saa hii. Tunamwona yule mjumbe wa saa hii. Tunamwona Mungu akijifunua Mwenyewe katika Neno Lake. Tunaona hakuna kitu kingine ila Ujumbe Huu, Mjumbe Huyu, Neno Hili.
Mwamini halisi hasikii kitu ila Neno. Hakuna zaidi. Yeye huliangalia Neno. Hatafuti mianya. Yeye hatafuti viinimacho. Anamwamini Mungu, na hilo latosha, naye anaendelea tu. Mnaona? Huyo hapo mwamini.
Sisi hatuwezi kusikia kitu kingine ila Neno; Neno linalomjia nabii peke yake. Si mianya, si fasiri ya mtu fulani, Neno Safi lililonenwa na kuwekwa kwenye kanda kwa ajili ya Bibi-arusi.
Roho amelihuisha Neno hilo ndani yetu nalo limekuwa hai. Kwa imani, tunaliona na kuliamini. Itakuja sauti kutoka Mbinguni ambayo italeta ubatizo mkubwa sana wa Roho Mtakatifu katika Bibi-arusi, ambao utatuondoa duniani, katika Neema ya Kunyakuliwa. Mungu aliahidi jambo hilo.
Tunawekwa majaribuni kila wakati, kila siku. Shetani anajaribu kutuambia majaribu na mitihani yetu ni Mungu anatuadhibu. Lakini MUNGU ASIFIWE, sivyo ilivyo, ni Shetani anayefanya jambo hilo naye Mungu analiruhusu.
Mungu anatujaribu, na kutufinyanga ili aone kile tutakachofanya. Jaribio huja kututikisa, kutuweka kule chini kabisa, kuona mahali tutakaposimama. Lakini tunashinda kila vita, kwa kuwa sisi ni mifano iliyo hai; Neno la Mungu linaishi ndani yetu na kupitia kwetu.
Sisi tuna umuhimu jinsi gani machoni pake?
Hakuna mtu anayeweza kupachukua mahali pako, haidhuru ni padogo namna gani. Unasema, “Mimi ni mke wa nyumbani tu.” Hakuna mtu anayeweza kupachukua mahali pako. Mungu, katika uchumi Wake mkuu, ameweka jambo hilo hivyo, Mwili wa Kristo, katika utaratibu, hata hapana mtu anayeweza kupachukua mahali pako.
Hilo ni lakupendeza jinsi gani? Kila mmoja wetu ana mahali. Kila mmoja wetu alikuwa hapa wakati Mungu aliponena ulimwengu ukawa. Aliweka mwili wetu hapa wakati huo huo. Mungu alituweka sisi duniani katika wakati huu ili kulitimiza Neno lake na kutupa Uzima wa Milele.
Kila mmoja anapaswa kufanya uamuzi. Unasimama wapi kuhusu Neno hili, Ujumbe huu, mjumbe huyu? Ni muhimu jinsi gani kulisikia Neno linalonenwa kwenye kanda?
Kwenye sehemu mbalimbali ulimwenguni, kanda hizi zinakopita, huduma za kanda.
Ni huduma ya kanda iliyotumwa kwa Bibi-arusi Wake ulimwenguni kote kutoka kwa Mungu. Inakuambia mahali ulipo hasa, wewe ni nani, na iwapo wewe ni mwamini katika Neno.
Wewe umo katika moja ya tabaka hizi. Katika hali yako ya sasa hivi, hali yako ya sasa ya akili, kwamba, ninyi mlio hapa katika mkutano huu unaoonekana, nanyi mtakaokuwa katika mikutano isiyoonekana ya kanda hii, hali yako ya sasa ya akili baada ya kuisikiliza kanda hii, inakuthibitishia uko katika tabaka gani.
Baada ya wewe kusikiliza kanda hii, inathibitisha uko katika tabaka la watu gani. Baadhi wanaamini unahitaji zaidi ya Neno safi tu lililonenwa kwenye kanda. Wengine wanaamini kwamba siku za Ujumbe wa mtu mmoja zimepita; ni lazima umsikilize mchungaji wako vinginevyo umepotea.
Mgawanyiko mkuu sana katika Ujumbe siku hizi ni umuhimu uliowekwa katika kuzisikiliza kanda. Baadhi wanafundisha kuwa ni makosa kuzicheza kanda kanisani; ni mchungaji pekee yake ndiye anayepaswa kuhudumu. Wengine wanasema kuna ulingalifu, lakini kamwe hawazichezi kanda kanisani, na kama wakizicheza ni mara chache sana.
Kulivyo na mitazamo mingi, mawazo mengi, fasiri nyingi za Neno, ni nani aliye sahihi? Ni yupi utakaye mwamini? Hilo ndilo swali ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza.
Nabii alituambia tulichunguze kwa NENO, sio yale mtu yeyote asemayo. unalifanyaje jambo hilo? KUNA NJIA MOJA TU PEKEE ya kufanya jambo hilo, BONYEZA PLAY.
Lazima kuwe na jibu sahihi, njia sahihi. Kila mtu lazima aamue mwenyewe. Jumapili hii itaamua wakati ujao wa wote wanaosikia Ujumbe huu.
Jambo unalopaswa wewe mwenyewe kujiuliza: Ni nani pekee aliye na Bwana Asema Hivi? Nguzo ya Moto ilimthibitisha nani? Ni nani atakaye tutambulisha kwa Yesu? Ni nani aliyenena Neno la kutokukosea? Ni maneno ya nani yaliyonenwa duniani yalikuwa muhimu sana, yakarudisha mwangwi mbinguni?
Iwapo ungependa kupata majibu sahihi, ningependa kukualika uje kusikiliza Jumapili hii saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville,( ni saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki ) kusikiliza Ujumbe: 63-1124E —Aina Tatu za Waamini.
Ndugu. Joseph Branham
Yohana Mtakatifu 6:60-71