UJUMBE: 60-1204M Ufunuo Wa Yesu Kristo
- 26-0712 Ufunuo Wa Yesu Kristo
- 24-1006 Ufunuo Wa Yesu Kristo
- 23-0416 Ufunuo Wa Yesu Kristo
- 20-1025 Ufunuo Wa Yesu Kristo
- 19-0106 Ufunuo Wa Yesu Kristo – Prliminari
- 16-0306 Ufunuo Wa Yesu Kristo
Wapendwa Tabaka La Watu Wa Kinabii,
Jinsi gani tunavyopenda neno, UFUNUO! Umuhimu wa Ufunuo WOTE wa Kweli kupitia Roho Mtakatifu kwa mwamini wa kweli hauwezi kamwe kutiliwa mkazo sana. Ufunuo ni zaidi ya maisha kwa Bibi-arusi; kwani juu ya MWAMBA HUU, UFUNUO, nitalijenga Kanisa langu, na kwa neema na rehema za Mungu, sisi ndilo Kanisa Lake lenye Ufunuo Wake wa Kweli.
Kitabu cha Ufunuo hakikukusudiwa kwa kila mtu. Hakuna mtu anayeweza kukielewa. Ni Kitabu cha kinabii kilichoandikwa kwa ajili ya, na kinaweza tu kueleweka na, tabaka la watu wa kinabii: SISI, Bibi-arusi wa Yesu Kristo.
Ndicho Kitabu pekee ambacho Kristo alikiandika Mwenyewe katika Biblia nzima, bali alikituma na kukionyesha kupitia malaika Wake kwa mtumishi Wake Yohana. Wanafunzi hawakuzijua kweli hizi zilizorekodiwa. Haikuwa imefunuliwa kwao hapo awali. Hata Yesu hakuweza kuwaambia kuhusu nafasi Yake Yeye ndani ya Hilo; kwani Baba alikuwa hajamfunulia Yeye hilo.
Lakini sasa, baada ya mauti na kufufuka Kwake, na katika wakati huu maalum, Yeye anaweza kumweleza Yohana Ufunuo huu wa Yeye Mwenyewe, kile utukufu Wake na uwepo katika kanisa ungemaanisha na kutenda.
Lakini hata sasa, baada ya miaka elfu mbili, ulimwengu umetafakari, wanatheolojia wamesoma na kuwazua, bali hakuna mtu aliye na fasiri sahihi na Ufunuo wa siri hizi zilizoandikwa katika Kitabu cha Ufunuo hadi leo hii, hadi wakati huu, ambapo Mungu alimtuma malaika yuyo huyo duniani ili kuyafunua yote Hayo kwetu sisi, Bibi-arusi Wake aliyemchagua.
Kujaribu kuelewa ukubwa wa kwamba Mungu alinichagua mimi, na Alikuchagua wewe; kuwa na Ufunuo wa Kweli wa Neno Lake yapita maelezo ya kibinadamu. Ingawa kuna wengi wanaodai wanaufuata Ujumbe na kusema wanaamini Mungu alimtuma nabii, wao hawana Ufunuo kamili kwa kujua matokeo ya kutoifanya Sauti Yake kuwa ndio sauti iliyo muhimu zaidi ambayo HAWANA BUDI KUISIKIA. Kuwa na Ufunuo huu wa Sauti Yake katika siku hii kweli ndio ile Lulu ya thamani kuu.
Mungu ametuchagua sisi kutufunulia huo UFUNUO WA KWELI. Hivyo basi, sisi ndilo KANISA Lake LA KWELI, jeshi Lake lisiloweza kushindwa ambalo Shetani hana nguvu mbele yalo, na kwa dhahiri atashindwa. Tukiwa na Ufunuo Wake wa Kweli maishani mwetu, malango ya kuzimu hayawezi kutushinda, bali tutayashinda. HAKUNA KITU kinachoweza kusimama mbele zetu.
Ufunuo wa Kweli na mkamilifu wa siku hii ni kutambua umuhimu wa Sauti ya Mungu ya siku yetu. Ikiwa kwenda kanisani, kuwa mshirika wa kanisa, kutoa dhabihu, kuomba, na kumwabudu Mungu ndio yote ambayo Mungu anayohitaji, basi Mungu angekuwa asiye haki kumhukumu Kaini kwa yeye kufanya kile alichosema afanye.
Hiki ndicho Sauti iliyo kwenye kanda inachomaanisha kwetu sisi:
Ufunuo wa kitu hicho chote umewekwa hapa nyuma pamoja na baraka kwa yeye alisomaye na kulisikia, pamoja na laana kwa hao watakaoongeza ama kutoa. Ni kitabu rasmi kikamilifu, loo, ile yakini. Hakuna kitu kinachoweza kuongezewa Kwake. Ndipo mtu anapojaribu kutoa chochote kutoka Kwake, au kuongeza chochote Kwake, Mungu alisema ataondoa sehemu iyo hiyo kutoka kwenye Kitabu cha Uzima. Mnaona? Angeondoa sehemu yake kutoka kwenye Kitabu, ikiwa angeongeza Kwake.
Kuliko hapo awali, Mungu ameiandaa NJIA KAMILIFU ya kutoongeza ama kutopunguza kutoka kwenye Neno Lake. Yeye ametupa fursa ya kuisikia Sauti Yake anaponena na kutufunulia sisi Neno Lake. Hakuwezi kabisa kuwa na kitu chochote kikuu zaidi ya hilo.
Huu ndio UFUNUO WA KWELI wa siku hii.
Nimesisimkwa mno na niko chini ya matarajio makubwa kwa yale yote Bwana aliyotuandalia tunaposikiliza, kusoma, na kujifunza Nyakati Saba za Kanisa. Mungu alikiandika, akamtuma malaika Wake kwa Yohana kumwonyesha Hicho, kisha akatusubiri sisi tuweze kuwa hapa duniani wakati huu hasa ili Yeye aweze kumtuma malaika yuyo huyo kwetu sisi kukifunua!
Hakujawahi kuwa na wakati mtukufu zaidi katika historia ya ulimwengu kuliko leo hii. Hakujawahi kuwa na heshima kubwa zaidi aliyowahi kupewa mwanadamu kuliko kupata fursa ya kuisikia Sauti ya Mungu wao wenyewe. Hakujawahi kuwa na wakati ambapo Bibi-arusi Wake angeweza kuungana pamoja kwa Sauti Yake wote kwa wakati mmoja.
Iweni tayari, Mungu anaenda kutupa Ufunuo zaidi kumhusu Yeye Mwenyewe na sisi ni nani: Jeshi Lake lisiloweza kushindwa, Bibi mteule, aliyechaguliwa, Kipenzi Chake ambaye amemngojea tangu mwanzo wa wakati.
Hakuna kinachoweza kutuondolea hilo. Limetia nanga katika mioyo na roho zetu zaidi ya hapo awali. Sasa limekuwa jambo halisi kwamba linatupa Imani Ya kunyakuliwa.
Tutaianza safari yetu kuu Jumapili hii saa 06:00 MCHANA, masaa ya Jeffersonville,(ni saa 1:00 JIONI ya Afrika Mashariki) tunapousikiliza Ujumbe wa kwanza: 60-1204M Ufunuo wa Yesu Kristo.
Nataka kukuhimiza ukitwae kitabu chako cha nyakati Saba za Kanisa, ukisome katika ukimya chumbani mwako na ujifunze, sura kwa sura, kila wiki. Tutaungana pamoja kuisikiliza Sauti Yake, kisha tujifunze Neno Lake.
Ndugu Joseph Branham