24-1110 Wakati Wa Kanisa La Thiatira

UJUMBE: 60-1208 Wakati Wa Kanisa La Thiatira

PDF

BranhamTabernacle.org

Mpendwa Bibi-arusi Aliyeangaziwa,

Jinsi ambavyo Bwana anavyotufunulia kwamba katika nyakati zote kumekuwa na kundi dogo sana ambalo lilidumu na Neno Lake. Wao hawakuanguka katika mtego wa udanganyifu wa adui, bali walibaki wa kweli na waaminifu kwa Neno la siku yao.

Lakini hakujawahi kuwa na wakati, au kundi la watu, ambalo Bwana amekuwa akijivunia, au kuwa na imani zaidi nalo, kuliko sisi. Sisi ndio Bibi-arusi Bibi Mteule Wake ambaye hatadanganywa, na hata muhimu zaidi HATUWEZI, kudanganywa; kwa maana sisi tunaisikia Sauti ya Mchungaji na kumfuata.

Yeye anatuonyesha kwamba katika nyakati zote kumekuwa na makundi mawili ya watu, yote yakidai ufunuo wao kutoka kwa Mungu na uhusiano wao na Mungu. Lakini alituambia, Bwana awajua walio Wake. Anafuatilia mawazo yetu. Yeye anajua kilicho mioyoni mwetu. Yeye anaziona kazi zetu kwa kudumu na nabii na Neno Lake, ambayo ni madhihirisho dhahiri ya yale yaliyo ndani yetu. Madhumuni yetu, makusudi yetu yanajulikana Kwake kwa kuwa Yeye hulichunguza kila tendo letu.

Yeye anatuambia kwamba ahadi zote alizozitoa kwa kila wakati, ni ZETU. Anatuona sisi tunaoendelea kutenda kazi Zake kwa uaminifu hata mwisho. Yeye AMETUPA SISI mamlaka juu ya mataifa. Anatuambia sisi ni viongozi wenye nguvu, hodari, shupavu ambao wanaweza kukabiliana vizuri sana na hali yo yote. Hata adui aliye mbaya sana atavunjwa kama kukiweko na haja. Dhihirisho letu la kutawala kwa mamlaka Yake litakuwa kama lile lile la Mwanawe. UTUKUFU!!

Tumepata ujuzi wa kina cha Mungu katika maisha yetu. Ni tukio la kibinafsi la Roho wa Mungu akiishi ndani yetu. Nia zetu zinaangazwa na hekima na maarifa ya Mungu kwa kupitia Neno Lake.

Sisi tunaenda po pote Bwana-arusi alipo. Hatutaachwa Naye kamwe. Hatutaondoka ubavuni Mwake. Tutashiriki kiti cha enzi pamoja Naye. Tutatiwa taji kwa utukufu na sifa Zake.

Yeye ametufunulia jinsi gani ambavyo adui amekuwa mdanganyifu katika kila wakati na jinsi ilivyo muhimu KUDUMU NA NENO LAKE LA ASILI. Hakuna Neno moja linaloweza kubadilishwa. Kila wakati waliongeza kwake na kuondoa kutoka kwake, wakiweka fasiri yao wenyewe kwenye Neno la asili; nao wanapotea milele kwa kufanya hivyo.

Katika Wakati wa Kanisa la Thiatira, hiyo roho ya udanganyifu ilinena kupitia papa wa Rumi na kulibadilisha Neno Lake. Alilifanya kuwa “mpatanishi mmoja kati ya Mungu na mwanadamu (si wanadamu).” Kwa hiyo sasa yeye anapatanisha kati ya mpatanishi na wanadamu. Hivyo, mpango wote wa Mungu ulibadilishwa; si kwa kubadili neno, bali kwa kubadili HERUFI MOJA. Shetani alikuwa amebadilisha “E” kuwa “A”.

Kila Neno litahukumiwa kwa Neno Lake la Asili lililonenwa kwenye kanda. Kwa hiyo, Bibi-arusi Wake LAZIMA adumu na kanda. Wakati adui anajaribu kuwakatisha tamaa watu kwa kuwapa mpango tofauti, wazo tofauti, herufi tofauti, Bibi-arusi ATADUMU NA NENO LA ASILI.

Katika kila wakati Yesu anajitambulisha Mwenyewe na mjumbe wa wakati huo. Wao wanapokea kutoka Kwake ufunuo juu ya Neno kwa ajili ya wakati wao. Ufunuo huu wa Neno huwaleta wateule wa Mungu kutoka katika ulimwengu na waingie katika muungano mkamilifu na Yesu Kristo.

Yeye amewaita na kuwaweka wakfu watu wengi ili wawe baraka kwa kanisa, lakini Yeye ana ila MJUMBE MMOJA TU ambaye Yeye alimuita ili KULIONGOZA kanisa Lake kwa Roho Wake Mtakatifu. Kuna SAUTI MOJA yenye Bwana Asema Hivi. Kuna SAUTI MOJA ambayo Yeye alisema atatuhukumu kwayo. Kuna SAUTI MOJA ambayo Bibi-arusi Wake wameweka kikomo chao cha Milele. SAUTI HIYO NI SAUTI YA MUNGU ILIYO KWENYE KANDA.

Bibi-arusi, Mapenzi ya Mungu kwetu ni Ukamilifu, na mbele zake, sisi NI WAKAMILIFU. Na huo ukamilifu ni subira, kumngojea Mungu… na kumngoja Mungu. Anatuambia ni njia ya kuumba tabia zetu. Tunaweza kuwa na mitihani, majaribu na dhiki nyingi, lakini uaminifu wako kwa Neno Lake unafanya subira ndani yetu ili tuwe wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa na neno.

Hatutasahau kamwe IMANI huja kwa kusikia, kusikia Neno, nalo Neno huja kwa nabii.

Njoo ujionee furaha kuu ya maisha yako unapoketi pamoja nasi katika Mahali pa Mbinguni tunapoisikia Sauti ya Mungu ikituletea Neno juu ya: Wakati wa Kanisa la Thiatira 60-1208, saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville.(Ni Saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki)

Ndugu. Joseph Branham