25-0126 Ufunuo, Mlango Wa Tano Sehemu Ya II

UJUMBE: 61-0618 Ufunuo, Mlango Wa Tano Sehemu Ya II

PDF

BranhamTabernacle.org

Wapendwa Wapumzikao,

Hakika haya ni Majira ya baridi yaliyo bora maishani mwetu. Kuja kwa Bwana kumekaribia. Tumetiwa muhuri na Roho Mtakatifu; Muhuri wa kibali cha Mungu kwamba kila kitu alichokifia Kristo ni mali yetu. 

Sasa tunayo arabuni ya urithi wetu, Roho Mtakatifu. Ni hakikisho, yale malipo ya kwanza, ya kwamba tumepokelewa katika Kristo. Tunapumzika katika ahadi za Mungu, tukilala katika joto la Mwangaza Wake wa Jua; Neno Lake lililothibitishwa, tukiisikiliza Sauti Yake.  

Ni arabuni ya wokovu wetu. Hatuna wasiwasi kama tunaenda kule ama hatuendi, TUNAENDA! Tunalijuaje hilo? Mungu alisema hivyo! Mungu aliliahidi nasi tunayo arabuni. Tayari tumeipokea na Kristo ametukubali.

Hakuna njia ya kuliondokea…kwa kweli, tupo hapo! Yote itupasayo kufanya ni kungojea tu; Yeye anafanya kazi ya Mkombozi wa Jamaa wa Karibu sasa hivi. Tunayo Arabuni yake sasa hivi. Tunangojea tu wakati ambapo Yeye atakaporudi kutuchukua. Kisha, katika dakika moja, katika kufumba na kufumbua jicho, sote tutakuwa tumekwenda kwenye Karamu ya Arusi.

Kuwazia tu yale yote yaliyo mbele yetu. Akili zetu haziwezi kuyaingiza yote ndani. Siku baada ya siku Yeye analifunua zaidi Neno Lake, akihakikisha kwamba ahadi hizi kuu ni zetu.

Ulimwengu Unaporomoka; mioto, matetemeko ya ardhi, na machafuko kila mahali, lakini wao wanaamini kuwa wanaye mwokozi mpya ambaye atauokoa ulimwengu, na kuwaletea wakati wao wa heri na furaha kuu. Tayari sisi tumekwishampokea Mwokozi wetu nasi tumekuwa tukiishi katika Wakati wetu wa Heri na Furaha Kuu. 

Sasa Yeye anatutayarisha kwa Ufunuo hata na zaidi wakati tunapoingia katika mlango wa 5 wa Ufunuo. Anaandaa tukio hapa kwa ajili ya kufunguliwa kwa ile Mihuri Saba. Kama tu vile alivyofanya katika mlango wa 1 wa Ufunuo, akiifungua njia kwa ajili ya Nyakati Saba za Kanisa.

Je! Majira mengine yaliyosalia ya baridi yatakuwaje kwa Bibi-arusi? Hebu tuangalie muhtasari mdogo:

Sasa, sina wakati. Nimeiandika, muktadha fulani juu yake hapa, bali mkutano wetu ujao kabla hatujaliingilia hili…Labda nitakapotoka kwenye likizo yangu ama wakati mwingine, ninataka kuyachukua haya majuma sabini ya Danieli na kuyafunganisha mumu humu, na kuonyesha mahali yanapolipeleka kwenye Yubile ya Pentekoste, na kuyarejesha moja kwa moja pamoja na vile ninii saba…hiyo mihuri saba itakayofunguliwa hapa kabla tu hatujaenda, na kuonyesha kwamba ni wakati wa mwisho, hii…

Ni wakati wa ajabu jinsi gani Bwana aliomwekea Bibi-arusi Wake. Akijifunua Mwenyewe katika Neno Lake kwetu zaidi ya hapo awali. Akitutia moyo kwamba sisi ndio wateule Wake anaowajia Yeye. Akituambia tuko katika mapenzi Yake Makamilifu kwa kukaa na Sauti Yake, na Neno Lake.

Tunafanya nini? Si hata jambo moja, tunapumzika tu! Tunangojea! Hakuna kutenda kazi tena, hakuna masumbuko tena, TUNAPUMZIKA KWENYE HILO!

Njoo upumzike pamoja nasi Jumapili hii saa 06:00 SITA MCHANA, saa za Jeffersonville, (Ni saa 2:00 MBILI USIKU ya Afrika Mashariki) tunapoisikia Sauti ya Mungu ILIYOTHIBITISHWA ikituletea Ujumbe: 

61-0618 – “Ufunuo, Mlango wa Tano Sehemu ya II”.

Ndugu. Joseph Branham